Thursday, July 11, 2013

Na Boniface Wambuea,

UGANDA CRANES YAWASILI KUIKABILI STARS, TENGA KUONGEA NA WANDISHI WA HABAR KESHO WAKATI WAJUMBE WA MKUTANO MKUU WAWASILI

WACHEZAJI WA TIMU YA UGANDA WAKIWASILI KATIKA UWANJA WA MWALUMU NYERERE JANA


TIMU ya soka ya taifa ya Uganda, The Cranes imewasili Dar es Salaam leo tayari kwa mechi ya kwanza ya mchujo kusaka tiketi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN) kati yake na Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
The Cranes inayofundishwa na Mserbia Sredojvic Micho imetua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 5.30 asubuhi kwa ndege ya Air Uganda, na imefikia hoteli ya Sapphire.
Timu hiyo leo (Julai 11 mwaka huu) itafanya mazoezi saa 9 alasiri kwenye Uwanja wa Karume, wakati kesho saa 9 alasiri itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, kabla ya kuipisha Taifa Stars itakayoanza mazoezi saa 10 kamili jioni.

Taifa Stars inayofundishwa na Mdenmark Kim Poulsen, na kudhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, leo kwa mujibu wa program yake haitakuwa na mazoezi.
Wachezaji wanaounda The Cranes ni makipa Ismail Watenga, Kimera Ali na Muwonge Hamza. Mabeki ni Guma Dennis, Kasaaga Richard, Kawooya Fahad, Kisalita Ayub, Magombe Hakim, Malinga Richard, Mukisa Yusuf, Savio Kabugo na Wadada Nicholas.
Viungo ni Ali Feni, Birungi Michael, Frank Kalanda, Hassan Wasswa, Kyeyune Said, Majwega Brian, Mpande Joseph, Muganga Ronald, Ntege Ivan, Owen Kasule, wakati washambuliaji ni Edema Patrick, Herman Wasswa na Tonny Odur.
Wakati huo huo: Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga atakuwa na mkutano na waandishi wa habari. Mkutano huo utafanyika kesho (Julai 12 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye hoteli ya Tansoma.
Kutokana na mkutano huo, sasa mkutano kati ya makocha wa Taifa Stars na The Cranes uliokuwa ufanyike saa 5 asubuhi ofisi za TFF nao umehamishiwa hoteli ya Tansoma. Mkutano huo pia utahusisha manahodha wa timu zote mbili.
Katika hatua nyingine, Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa TFF utakaofanyika Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) wanawasili jijini Dar es Salaam kesho (Julai 12 mwaka huu).
Mkutano huo wa marekebisho ya Katiba utakuwa chini ya uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga na utafanyika ukumbi wa NSSF Waterfront kuanzia saa 3 kamili asubuhi. Wajumbe wote wa mkutano huo watafikia hoteli ya Travertine.
Pia mkutano huo utahudhuriwa na wageni mbalimbali waalikwa wakiwemo kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).
Na mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Stand United FC ya Shinyanga na Kimondo SC ya Mbeya iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) imesogezwa mbele kwa siku moja.
Timu hizo sasa zitacheza Jumapili (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Kimondo ilishinda bao 1-0 mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 6 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi nyingine ya ligi hiyo itakuwa kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na Polisi Jamii ya Mara, na itafanyika kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Mwamuzi wa mechi hiyo ni Hans Mabena kutoka Tanga.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu