Friday, July 26, 2013

RAIS KIKWETE A AMEAMURU MAJAMBAZI NA WAHAMIAJI KUCHUKULIWA HATUA





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho ameamuru majambazi na wahamiaji haramu wote katika mikoa mitatu nchini kujisalimisha katika muda wa siku 14 kuanzia leo, Ijumaa, Julai 26, 2013 kabla ya kuanza kwa operesheni kubwa kuliko zote katika historia ya Tanzania nyenye lengo la kukomesha ujambazi katika mikoa hiyo na kukamata wahamiaji haramu.

Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu amesema kuwa leo ametoa amri kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama nchini kuanza maandalizii ya operesheni hiyo na hatimaye kuiendesha katika Mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.

Majambazi wanateka magari, wanaua watu wetu, wanapora mali zao. Watanzania hawawezi kuendelea kuishi kwa hofu, woga na taabu katika nchi yao wenyewe. Tutawasaka majambazi misituni, tutawasaka majumbani, tutachimbua ardhini kutafuta hata silaha zilizofukiwa chini,” amesema Rais Kikwete.

Rais Kikwete ametoa amri hiyo mchana wa leo, Ijumaa, Julai 26, 2013 wakati alipohutubia wananchi wa mjini Biharamulo, Mkoani Kagera, kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kagoma, Wilaya ya Muleba kwenda Lusahuga, Biharamulo.

Rais Kikwete ametoa amri hiyo kufuatia matukio ya mara kwa mara na yasiyokuwa na mwisho ya majambazi kuteka mabasi, kuua watu na kupora mali zadi katika mikoa hiyo, hali ambayo imesababisha malalamiko ya wakazi wa mikoa hiyo.

Rais Kikwete ameaambia wananchi: “Tumeamua kukomesha upuuzi huu katika mikoa ya Kagera, Kigoma Geita. Leo nimetoa maagizo kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama – Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Usalama wa Taifa kuandaa operesheni maalum, operesheni kubwa kuliko zote tokea tupate uhuru. Upuuzi huu hauwezi kuendelea.”

Ameongeza Rais Kikwete na kuwaambia wananchi: “Nawaamuru majambazi wote, wenye kumiliki silaha kinyume cha sheria na wahamiaji haramu wote wajisalimishe katika wiki mbili kuanzia leo. Wajisalimishe wao pamoja na silaha zao. Baada ya hapo, tunaanzisha operesheni ambayo haijapata kuonekana katika historia ya nchi yetu.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Sitanii, sina mzaha na hili. Nimechoka. Nalisema hili mchana, macho makavu. Nawaambia majambazi watafute kazi nyingine, kazi hii hailipi tena. Kwa wale majambazi na wahamiaji haramu kutoka nchi za jirani, waanze safari ya kurejea kwao.”

Rais Kikwete ameonya: “Na hata wale wanaoishi na kulea majambazi na wahamiaji haramu nao wajisalimishe. Na ole wao majambazi watakaojaribu kuwapiga risasi askari wetu. Watakiona cha mtema kuni.”

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu