Monday, September 2, 2013

HENRY JOSEPH AITWA TAIFA STARS

 

Na Boniface Wambura, 
I
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen amemjumuisha kiungo Henry Joseph wa Simba kwenye kikosi chake kinachojiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul.
Kwa miaka miwili sasa kiungo huyo na nahodha wa zamani wa Taifa Stars hajaitwa timu ya taifa, lakini nyota yake imeng'ara tena baada ya kurejea Msimbazi.
Tayari Joseph amekwisharipoti kwenye kambi ya timu hiyo iliyoko hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam. 
Henry amerejea Simba ASC msimu huu baada ya kuitumikia Kongsvinger ya Norway tangu mwaka 2009 alipojiunga nayo akitokea kwa Wekundu hao wa Msimbazi.

Taifa Stars ambayo iko chini ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini tangu Agosti 29 mwaka huu, na leo jioni itafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Programu ya timu hiyo inaonesha kuwa kesho (Septemba 3 mwaka huu) itafanya mazoezi yake asubuhi na jioni kwenye uwanja huo huo wa Kumbukumbu ya Karume.
Kesho Saa 6:00 mchana Kocha Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa mikutano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam.
Wakati huo huo: Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limemteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa mtathmini wa waamuzi kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Coton Sport ya Cameroon na Esperance ya Tunisia.
Mechi hiyo ya kundi B itachezwa Septemba 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa Omnisport Roumdeadjia mjini Garoua, Cameroon. Kamishna atakuwa Bema Doumbia wa Ivory Coast.
Waamuzi wanatoka Madagascar wakiongozwa na Hamada Nampiandraza. Wasaidizi wake ni Jean Eric Pierre Andrivoavonjy, Ferdinand Velomanana Linoro na Bruno Marie Andrimiharisia.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu