Wednesday, September 25, 2013

Maafa! Kanisa lalipuliwa na kuua watu 75, zaidi 100 hoi

 
WAUAJI  wawili wa kujitoa mhanga wamelipua mabomu yao nje ya kanisa la kihistoria nchini Pakistan jana na kuua watu 75 kwenye shambulio baya zaidi kuwahi kutokea kwa Wakristo walio wachache wa nchini humo.
Taliban wa Pakistan wamekiri kuhusika na shambulio hilo lililotokea katika mji wa Peshawar, wakisema wataendelea kuwalenga wasio Waislamu hadi hapo Marekani itakapositisha mashambulizi katika mji huo wa kikabila nchini humo. 



Shambulio la hivi karibuni lilifanyika Jumapili pale makombora yalipopiga majengo mawili katika eneo la North Waziristan, na kuua watu sita wanaodhaniwa kuwa wanamgambo, maofisa wa intelijensia Pakistan walisema.
Shambulio kwenye Kanisa la All Saints, ambalo pia lilijeruhi watu 110, linatekeleza kitisho kilichotolewa na Taliban wa Pakistan wakati huku serikali ikitaka mpango wa amani na wanamgambo hao.
Shambulio hilo limetokea wakati mamia ya waumini wakiwa wanatoka nje ya kanisa hilo lililoko katika wilaya ya Kohati Gate mjini humo baada ya huduma ya kupata chakula cha bure aina ya wali.
"Kulikuwa na milipuko na kulikuwa na mateso kwetu sote," alisema Nazir John, ambaye alikuwa kanisani pamoja na takribani waumini wengine 400.
"Niliporejewa na fahamu zangu, sikuona chochote ila moshi, vumbi, damu na watu waliokuwa wakilia kwa uchungu. Niliona sehemu za miili zilizosambaratika na damu kuzunguka eneo lote."
Manusura walikumbatiana kila mmoja baada ya milipuko huko. 
Ukuta mweupe wa kanisa hilo, ambalo lilifunguliwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa miaka ya 1800, ulitapakaa mashimo yaliyochimbwa na vipande vya vyuma vilivyotoka katika mabomu ma kusababisha uharibifu mkubwa.
Damu ilitapakaa sakafuni na kusambaa kwenye ukutani. Sahani zenye wali zilitawanyika kila pembe za eneo hilo.
Shambulio hilo lilifanywa na watuhumiwa wawili wa kujitoa mhanga ambao walilipua mabomu yao kwa kupokezana. Mamlaka zimekuta sehemu za mwili na zilikuwa zikijaribu kutambua umri wao.
Milipuko hiyo imeua watu 75 na kujeruhi wengine 110. Waliokufa ni pamoja na wanawake na watoto.
Idadi ya majeruhi ni kubwa mno kiasi cha hospitali hiyo kuishiwa majeneza kwa ajili ya waliokufa na vitanda kwa ajili ya majeruhi, alisema Mian Iftikhar Hussain, waziri wa zamani wa habari wa jimbo la Khyber Pakhtunkhwa ambaye alikuwa katika eneo la tukio.
"Hili ni shambulio baya zaidi dhidi ya Wakristo katika nchi yetu," alisema Irfan Jamil, askofu wa mji wa mashariki wa Lahore.
Mmoja wa waliojeruhiwa, John Tariq, ambaye amepoteza baba yake katika shambulio hilo, aliwauliza washambulizi hao, "Tumewakosea nini watu hawa? Kwanini tumekuwa tukiuawa?"
Ahmad Marwat, ambaye alijitambulisha kama msemaji wa tawi la Jundullah la Taliban wa Pakistan, alidai kuhusika na shambulio hilo.
"Wote wasio Waislamu nchini Pakistan ni walengwa wetu na wataendelea kuwa hivyo kwa wakati wote Marekani inaposhindwa kusitisha mashambulizi katika nchini yetu," alisema Marwart kwa njia ya simu kutoka sehemu isiyojulikana.
Askofu wa Peshawar, Sarfarz Hemphray, ametangaza siku tatu za maombolezo kufuatia shambulio hilo na kuishutumu serikali na vyombo vya ulinzi kwa kushindwa kuwalinda Wakristo wa nchini humo.
"Endapo serikali itaonesha nia, inaweza kudhibiti ugaidi huu," alisema Hemphray. "Tumekuwa tukizitaka mamlaka kuimarisha ulinzi, lakini hazitilii maanani."
Waziri Mkuu wa Pakistani ameshutumu shambulio hilo katika taarifa iliyotumwa kwa waandishi wa habari, akisema, "Magaidi hawana dini na wanaolenga watu wasio na hatia ni kinyume cha mafundisho ya Kiislamu na dini zote."
"Matukio kama hayo ya kiwendawazimu ya ugaidi yanaakisi unyama na akili zisizo za kibinadamu za magaidi," alisema.

Wawili wanaswa na maiti yenye dawa za kulevya

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na maiti, iliyokuwa na pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin tumboni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova alitaja waliokamatwa kuwa ni Nasri Omari (36), maarufu kama Rajabu Robot na Mwanaisha Salim( 36), mkazi wa Kigogo Luhanga.

“Kila pipi ina urefu wa sentimita sita...tulipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa huko Tabata kuna mtu mmoja alifariki ghafla muda mfupi baada ya kutoka bafuni kuoga na tukaamua kulifuatilia tukio hilo” alisema.

Alisema makachero walifika eneo la tukio, nyumbani kwa Omari na kuhoji hatimaye kugundua uwepo wa maiti sebuleni ikiwa imelazwa chali katika godoro sakafuni huku akiwa hana nguo na amefunikwa na shuka.

“Omari ambaye ndiye mmiliki wa chumba kilichokutwa maiti, alisema marehemu anajulikana kwa jila la Rajabu Kandunda (43), maarufu kama Mashaka Mabruki” alisema.

Kamishna Kova alisema uchunguzi wa awali, ulionesha kuwa Kandunda alifika kutoka Mtwara Septemba 21 kwa maelezo kwamba alikuwa mgonjwa na alikwenda kuchukuliwa na watuhumiwa hao wawili.

Alisema uchunguzi huo, ulifanywa na jopo la madaktari wawili na kushuhudiwa na maofisa wa juu wa Polisi na ndugu wa karibu wa marehemu, ambapo katika uchunguzi huo wa mwili wa marehemu, tumboni zilikutwa pipi 33 za dawa za kulevya aina ya heroin, zenye thamani ya mamilioni ya fedha.

“Zipo taarifa zinazoonesha kwamba alikuwa ni mhalifu mzoefu wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kwani kabla ya kurudi Tanzania alikuwa akitumikia kifungo nje ya nchi barani Asia” alisema.

Kova alisema uchunguzi zaidi unafanyika ili kujua mtandao mzima wa usafirishaji wa dawa hizo, ambao umemhusisha marehemu. Alisema wote watakaobainika kuhusika, watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha alisema baada ya upekuzi, marehemu huyo alikutwa na vielelezo vingine, ikiwemo fedha za Kenya Sh 700, Dola za Marekani 100 na fedha ya Ushelisheli.

Alisema operesheni ya kukamata dawa za kulevya, inaendelea. Aliomba raia wema kuendelea kutoa taarifa za dawa hizo, kwani zina madhara makubwa kwa wananchi, hasa vijana

Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu