Friday, September 27, 2013

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR ATEMBELEA TANGA NA DAR

 Baadhi ya Wazanzibari wanaoishi Tanga wakimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika ukumbi wa Tangamano jijini Tanga, leo  (picha na Salmin Said, OMKR)

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akiwapungia mkono wananchi wakati akitoka katika ukumbi wa hoteli ya Starlight jijini Dar es Salaam, baada ya kuzungumza na Wazanzibari wanaoishi Dar es Salaam.jana (picha ya Salmin Said, OMKR.

 Baadhi ya Wazanzibari wanaoishi Tanga wakimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika ukumbi wa Tangamano jijini Tanga, LEO



DAR ES SALAAM      NA TANGA                               
Wazanzibari wamehimizwa kuitumia vyema fursa ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, ili waweze kushiriki katika maamuzi yanayohusu nchi yao.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, alipokuwa akizungumza na Wazanzibari wanaoishi Dar es Salaam katika mkutano uliofanyika hoteli ya Starlight jijini Dar es Salaam.
Amesema wakati mchakato wa kulifanyia uhakiki daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuandikisha wapiga kura wapya  ukiendelea Zanzibar, bado kuna idadi ndogo ya wanaojitokeza kujiandikisha ikinganishwa na tathmini ya Tume ya Uchaguzi.
Amesema ili kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki katika maamuzi yanayohusu Zanzibar likiwemo suala la kura ya maoni kwa ajili ya kupitisha au kukataa katiba mpya, hawana budi kujiandikisha katika daftari la kudumu ili waweze kuitumia haki hiyo ya kupiga kura.
Ametoa wito kwa wananchi wenye sifa kujiandikisha katika  daftari la kudumu la wapiga kura, ili waweze kuitumia haki yao hiyo ya kidemokrasia.
Akizungumzia kuhusu mchakato wa kuandika katiba mpya ya Tanzania, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF amesema bado hajaridhishwa na baadhi ya vipengele vilivyomo katika mswada wa sheria inayohusu marekebisho ya Katiba, ambapo Serikali pamoja na asasi za kiraia Zanzibar hazikushirikishwa katika marekebisho hayo.
Amesema katiba ni jambo kubwa linaloeleza mustakbali wa taifa kwa kipindi kirefu, hivyo kufikia pahala ikapitishwa kwa ushindi mdogo (just simple majority), halitokuwa jambo la busara kwa mustakbali wa Taifa.
Amefahamisha kuwa wakati mchakato huo wa katiba ukiendelea ni vyema kwa washirika wa Muungano kuwa na fursa sawa kama nchi, hasa katika ushiriki wa wajumbe kwenye Bunge la Katiba.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Ole (CUF), Hamad Massoud Hamad amesema takwimu za uandikishaji katika daftari hilo ambao umekamilika kwa upande wa Unguja zinaonesha kuwa idadi kubwa ya wananchi hawakujitokeza katika uandikishaji huo.
Amedai kuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ilitarajia kuandikisha zaidi ya wapiga kura laki moja kwa Wilaya sita za Unguja, lakini hadi zoezi hilo linakamilika ni asilimia 23 ya wananchi waliojitokeza kuandikishwa.
Wakati zoezi hilo likikamilika kwa upande wa Unguja, linatarajiwa kuanza rasmi katika Wilaya nne za Pemba ambapo watu wapatao 52 elfu wanatarajiwa kusajiliwa.
Zoezi hilo litakaloanzia Wilaya ya Micheweni tarehe 12/10/2013, litakuwa likifanyika siku tatu kwa kila shehia.
Amewasisitiza wananchi wenye sifa kutopuuza fursa hiyo, kwani kuwa na Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (ZAN ID) na kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, ni fursa za kipekee katika kushiriki masuala ya kitaifa na maendeleo kwa ujumla.
Mapema akisoma risala ya Jumuiya ya Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara, Said Rashid Salum amesema watashirikiana na wazanzibari popote walipo katika kutetea haki na maslahi ya Zanzibar katika Nyanja zote za kimaendeleo.
Mkutano kama huo unatarajiwa kufanyika katika Mkoa wa Tanga, tarehe 27/09/2013.

Hassan Hamad (OMKR).

Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu