Malkia wa Zouk nchini Hafsa Kazinja
akiwa na Omari Mkali (kushoto) na Abdul Salvador baada ya kukamilisha kurekodi
wimbo wa 'NIMUOKOE NANI' katika Studio za OM Productions jijini Dar es salaam
wikiendi hii.
Baada ya ukimya wa muda mrefu,
Malkia wa Zouk Tanzania, Hafsa Kazinja, anaibuka
upya katika fani akiwa na ingizo lake la kwanza kati ya kumi aliyoandaa
kwa kuimba wimbo maarufu wa NUTA Jazz Band uitwao “NIMUOKOE NANI”
anauouleta hewani katika mahadhi ya Zouk.
Hafsa Kazinja anasema ameamua kurudi
ulingoni kwa kutoa wimbo huo ili kumuenzi Mzee Muhidin Maalim Gurumo ambaye
amestaafu rasmi fani ya muziki baada ya kufanya kazi hiyo akiwa na bendi
mbalimbali tokea mwaka wa 1960.
“Nimeamua kuimba wimbo huu wa
“NIMUOKOE NANI” ili kumuenzi gwiji huyu wa muziki kwani wakati yeye
anastaafu na mimi ndiyo naibuka upya baada ya kukaa kimya kwa muda”, anasema
Hafsa ambaye alitoka kwa wimbo wake wa “PRESHA” aliomshirikisha Banana Zorro.
Hafsa ameandaa wimbo huo wa “NIMUOKOE
NANI” katika studio za OM Productions ya jijini Dar es salaam chini ya
wanamuziki nguli, Abdul Salvador na Omari Mkali.
“Nafurahi kwamba wimbo wa NIMUOKOE
NANI nimeuimba baada ya kupata Baraka zote toka kwa mtunzi na mwimbaji wake
Mzee Gurumo mwenyewe.
“Haikuwa rahisi kama inavyoweza
kudhaniwa kwani baada ya kwenda kumuona nyumbani kwake alinifanyisha mtihani wa
kuuimba wote kabla ya kuridhika maana alisema asingefurahi kuona wimbo wake
unaimbwa hovyo hovyo na kuharibiwa radha yake”, anasema Hafsa, ambaye hivi sana
anamalizia ngoma zake zingine tisa alizotunga mwenyewe, kabla ya kuvamia anga
kwa mara ingine.
Hafsa anasema katika ukimya wake
amekuwa akifanya utafiti na kujifunza kwa undani zaidi fani ya muziki, akipata
mawaidha maridhawa toka kwa wanamuziki nguli ndani nan je ya nchi wakiwemo
Muhidin Maalim Gurumo, Omar Mkali, Abdul Salvador na Lokassa ya Mbongo wa Congo
aliyekutana na kufanya naye kazi alipokuwa ziarani Marekani hivi karibuni.
Msanii huyu wa kizazi kipya anasema
ataitambulisha rasmi ngoma ya “NIMUOKOE NANI” katika tamasha la kumuenzi Mzee
Gurumo lililopangwa kufanyika OKtoba 1, 2013 katika ukumbi wa Diamond Jubilee
jijini Dar es salaam.
“Natumaini wapenzi wa muziki
watafurika kwa wingi kwenye tamasha hilo name naahidi kuitendea haki ngoma ya
“NIMUOKOE NANI” hivyo wasikose kuja kujionea wenyewe jinsi sie wa kizazi kipya
tunavyoweza kufanya kazi na wakubwa wetu wa kazi, anaongezea Hafsa ambaye pia
anaandaa video yake pamoja na ya ngoma zake zingine mpya.
Mkongwe Abdul Salvador, ambaye alikuwa
mmoja wa waanzilishi wa bendi ya TANCUT ALMASI YA Iringa iliyotamba na
mtindo wake wa “FIMBO LUGODA”, anamtaja Hafsa kazinja mmoja wa wanamuziki wa
kike waliojaaliwa sauti nzuri na kipaji cha hali ya juu hapa nchini.
“Kwa kuweza kuimba wimbo wa Mzee Gurumo
na kupatia kisawasawa inadhihirisha kwamba Hafsa ni mwanamuziki aliyekomaa
maana si mchezo kuimba nyimbo ya wakongwe kwa ufasaha kama alivyofanya Hafsa.
“Na hii inadhihirisha kwamba
uwezekano wa kizazi kipya na cha zamani kufanya kazi pamoja ni mkubwa sana na
sioni kwa nini isiwe hivyo”, anasema Salvador.
Omari Mkali, aliyetamba na bendi ya
CHUCHU SOUNDS, chini ya marehemu Yusuf Chuchu, naye anamwelezea Hafsa Kazinja
kama moja ya majembe ya muziki hapa nchini kwa upande wa kinamama, na kwamba
anaweza kufika mbali endapo kama moto aliokuja nao upya atauendeleza.
IMETOLEWA NA
OM PRODUCTIONS NA HISIA SOUNDS
CODES ZA STUDIO:
0 comments:
Post a Comment