“Nimeshtushwa,
nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya watu 13 akiwemo mtoto
wa miezi minne waliofariki papo hapo katika eneo la ajali tarehe 20 Januari,
2014 baada ya gari aina ya Toyota Noah walilokuwa wakisafiria kutoka Itigi kwenda
Singida kugongana uso kwa uso na lori katika eneo la Isuna”.
Rais Kikwete
amesema inatia simanzi kuona ajali zikiendelea kutokea na kupoteza maisha ya
watu wasio na hatia na hususan mtoto mdogo kama huyu wa miezi minne,
kusababisha ulemavu wa kudumu kwa baadhi ya watu na uharibifu wa mali kutokana
na makosa ya binadamu katika uendeshaji wa vyombo vya moto.
“Kufuatia
ajali hiyo ya kusikitisha, ninakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa
Perseko Kone salamu zangu za rambirambi kutokana na msiba huo, na kupitia
kwako, naomba unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa familia
zote zilizopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Nawaomba wanafamilia wawe na
moyo wa uvumilivu, subira na ujasiri hivi sasa wanapougulia machungu ya kupotelewa
na ndugu zao”,
amesema Rais Kikwete kwa masikitiko.
Aidha Rais
Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza
Mahala Pema Peponi Roho za Marehemu wote, na amewahakikishia wafiwa kuwa yuko
pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa.
Vilevile
amemtakia ahueni kijana mmoja majeruhi wa ajali hiyo na aweze kupona haraka na
kurejea katika hali yake ya kawaida na kuungana tena na ndugu na jamaa zake.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
20
Januari, 2014
0 comments:
Post a Comment