Thursday, May 1, 2014

HALMASHAURI NA WADAU WA JIJI LA MWANZA WAANZA MAANDALIZI YA SHEREHE ZA KUADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA ZITAKAZOFANYIKA JUNI 16.

Halmashauri pamoja na wadau toka mashirika na taasisi za kutetea na kulinda haki za watoto jijini Mwanza wameanza rasmi vikao vya maandalizi ya kuadhimisha sherehe za siku ya mtoto wa Afrika inayoadhimishwa kila Mwaka Juni 16.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri wa Jiji la Mwanza chini ya Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo Bi. Eluminatha Mwita wajumbe walikubaliana kuadhimisha siku hiyo katika Kata ya Buhongwa, kwa Wilaya ya Nyamagana.

Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu, na umuhimu wa mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanywa kila juni 16 tangu ilipotangazwa kuwa siku rasmi mwaka 1991 na jumuiya ya umoja wa Afrika.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho Afisa Maendeleo Jamii wa Jiji la Mwanza Bi. Eluminatha Mwita alisema kuwa kauli Mbiu ya mwaka huu ni “Kuondoa Mila Zenye Kuleta Madhara kwa Watoto ni Jukumu Letu Sote” na kufafanua kuwa kauli hiyo inalenga kuwasisitiza wazazi na walezi kuacha mila potofu zenye kuleta madhara kwa watoto.

Bi Eluminatha alisema kuwa “Kauli mbiu hiyo ina lenga kuangalia mila zote kandamizi na potofu zinazotokana na jamii husika katika malezi ya mtoto na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa watoto wa mitaani, kubakwa kwa watoto, kukosa elimu, afya na malezi bora pamoja na vifo kwa watoto hawa”.

Kikao hicho cha kwanza kiliweza kuchagua viongozi wa kamati hiyo ya maandalizi, mwenyekiti aliyechaguliwa ni Godfrey Salum huku katibu ni Devis Mrope na katibu msaidizi akichaguliwa Francisca Michael, baada ya kupata viongozi kamati nne ziliundwa na wajumbe, Kamati ya Uratibu, Mipango na Fedha, Kamati ya Usafiri na Ulinzi, Kamati ya Mapambo na Burudani pamoja na kamati ya Hotuba na Habari.

Imeandaliwa na Afisa Habari wa Kamati ya Maandalizi
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika - Mwanza
Hassan Mrope

***********************************************

           
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu