Rais was Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wake wakiongea na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria Mheshimiwa Abdelmalek Sellal alipowasili
mjini Algiers, mji mkuu wa Algeria, mchana wa leo, Jumamosi, Mei 9,
2015 kuanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku tatu katika nchi hiyo
rafiki wa miaka mingi wa Tanzania kwa mwaliko wa Rais Abdelaziz
Bouteflika.
PICHA NA IKULU
Rais was Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Algiers,
mji mkuu wa Algeria, mchana wa leo, Jumamosi, Mei 9, 2015 kuanza ziara rasmi ya
Kiserikali ya siku tatu katika nchi hiyo rafiki wa miaka mingi wa Tanzania kwa
mwaliko wa Rais Abdelaziz Bouteflika.
Rais Kikwete
amewasili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria akitokea New York,
Marekani, ambako kwa wiki nzima amekuwa anaendesha vikao vya Jopo la Watu
Mashuhuri Duniani ambao wanatafuta jinsi gani dunia inaweza kujiandaa vizuri
zaidi kukabiliana na majanga ya afya, na hasa magonjwa ya milipuko, katika siku
zijazo kufuatia balaa la ugonjwa wa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi za
Guinea, Liberia na Sierra Leone.
Kwenye Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Houari Boumediene mjini Algiers, Rais Kikwete amepokelewa
na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria Mheshimiwa
Abdelmalek Sellal kabla ya kuelekea kwenye Kasri ya Kirais ya Zeralda ambako
amefikia.
Baadaye jana jioni,
Rais Kikwete ameweka shada la maua kwenye Mnara wa Taifa kwa heshima ya
wanamapinduzi waliopoteza maisha yao katika vita vya ukombozi wa kuwania uhuru
wa Algeria kutoka kwa Wafaransa.
Algeria ilipata uhuru
kutoka kwa Wafaransa mwaka 1962 baada ya vita kali ya ukombozi ya miaka minane,
ambako pia wananchi wanaokadiriwa milioni mbili walipoteza maisha yao.
Baadaye, Rais Kikwete
pia amembelea Jumba la Makumbusho la Mashujaa wa Vita ya Ukombozi mjini Algiers.
Kesho, Jumapili, Mei
10, 2015, Rais Kikwete atahudhuria dhifa ya kitaifa ambayo itaandaliwa kwa
heshima yake na Waziri Mkuu ambaye atafanya naye mkutano rasmi kabla ya dhifa.
Baadaye, Rais
atakwenda kwa mazungumzo rasmi ya Kiserikali na Rais Abdelaziz Bouteflika,
ambaye mwaka jana alichaguliwa tena kwa mara ya nne kuongoza Algeria tokea
alipochaguliwa kuwa Rais kwa mara ya
kwanza mwaka 1999 baada ya kutumikia kama Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi yake
kwa miaka mingi. Tokea 1999, alichaguliwa tena 2004, mwaka 2009 na mwaka jana.
Tanzania
na Algeria zimekuwa marafiki wa karibu kwa miaka mingi tokea uhusiano
ulipoanzishwa na waanzilishi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwalimu Julius
Nyerere na Hayati Ben Bella. Kwa hakika, Algeria ilikuwa moja ya nchi chache
duniani zilizoisaidia sana Tanzania wakati wa Vita ya Kagera dhidi ya Idi Amin.
Tanzania pia imekuwa
inapata misaada mikubwa kutoka Algeria katika sekta za gesi a elimu na katika
kitendo kilichothibitisha ukaribu kati ya Tanzania na Algeria, mwaka 2010,
Algeria iliifutia Tanzania kiasi cha dola za Marekani milioni 144. Kiasi hicho
kilikuwa ni pamoja na deni la awali la dola milioni 58.03, deni ambalo
liliongezeka kwa sababu ya mikopo ya mafuta ambayo Tanzania ilikuwa inapata
kutoka Algeria na riba.
|
0 comments:
Post a Comment