Friday, May 6, 2016


BILIONI 6 ZA RAIS DK. JOHN MAGUFULI KUNUNULIA MADAWATI ZAIBUA MAJIPU JESHINI
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Edosama Wood,  Research Center cha Kinyerezi jijini Dar es Salaam, Edward Maduhu (katikati), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, akidai kutapeliwa na maofisa wa jeshi la Magereza na Kujenga Taifa (JKT), katika utengenezaji wa madawati ya bei nafuu kama Rais Dk. John Magufuli alivyoagiza.
Maduhu akiwaonesha waandishi wa habari picha mbalimbali walizopiga na maofisa wa majeshi hayo walipofika kufanya kikao na uongozi wa kiwanda hicho.
Maduhu akionesha madawati yanayotengenezwa na kiwanda chake.
Moja ya mashine zinazotumika kutengeneza samani mbalimbali katika kiwanda hicho.

Na Dotto Mwaibale

SHILINGI bilioni 6 zizotengwa na Rais Dk.John Magufuli kwa ajili ya utengenezaji wa madawati zimeibua majipu katika Jeshi la Magereza na Kujenga Taifa (JKT), kwa kudaiwa kumtapeli Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Edosama Wood,  Research Center cha Kinyerezi jijini Dar es Salaam, Edward Maduhu katika utengenezaji wa madawati.

 Maduhu  amezilalamikia taasisi hizo za jeshi akidai zimemtapeli katika kazi ya kutengeneza madawati hayo baada ya kukubaliana kufanya ushirikiano wa kazi hiyo kufuatia wao kuelemewa.

Maduhu alitoa lawama hizo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kutapelewa na majeshi hayo waliofika kiwandani kwake kuomba ubia wa kushirikiana kutengeneza madawati ya bei nafuu kama alivyoagiza Rais.

Hata hivyo, Mkuu wa Kiwanda cha Magereza, ACP Ismail Mlawa, alisema baada ya serikali kutoa ‘order ya kutengeneza madawati hao, taasisi hizo mbili ziliunda timu maalumu ya kutengeneza madawati hayo.

Alisema, baada ya kuunda timu hiyo, walikubaliana kuzunguka kwenye viwanda mbalimbali nchini kwa ajili ya kuangalia vifaa na sampuli ya utengenezaji wa madawati hayo ili yaweze kuwa katika ubora unaokubalika.

Alisema, kutokana na hali hiyo, timu hiyo ilikwenda kwenye viwanda mbalimbali kikiwamo hicho cha Edosama kwa lengo la kuangalia upatikanaji wa vifaa na si vinginevyo.

“Tulienda kwenye viwanda zaidi ya vinne kikiwamo cha Edosama, lengo ni kuangalia namna ya upatikanaji wa ‘material’ (vifaa) vya kutengeneza madawati pamoja na kufanya ‘window shoping’ lakini katika viwanda vyote hivyo, hakuna hata kimoja tulichoingia nacho mkataba wa kutengeneza madawati kwa sababu hatukuwa na mamlaka ya kufanya hivyo mpaka tutakapowasilisha taarifa kwa viongozi wetu,”alisema Mlawa.

Aliongeza, baada ya kuona wanavyotengeneza madawati hao, walilazimika kuwasilisha taarifa hiyo kwa viongozi wao ili waweze kujadiliana kuhusiana na suala la utengenezaji wa madawati hao.

Maduhu alisema Aprili 12 mwaka huu walipigiwa simu na maofisa wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza ambao walifika katika kiwanda chao na kufanyanao vikao vinne kuanzia Aprili 12 na 15 mwaka huu.

Alisema maofisa wa majeshi hayo walioshiriki vikao hivyo ni Kanali Wanyancha na Tendwa Mahunnah wote kutoka JKT na ASP Mlawa pamoja na ofisa mwingine wa Jeshi la Magereza ambaye jina lake halikupatikana.

Maduhu alisema kwamba katika kikao hicho jumla walikuwa saba pamoja na maofisa wa kiwanda hicho na kuwa katika kikao hicho walifanikiwa kupiga picha za mnato, kurekodi mazungumzo yote.

Aliongeza kuwa katika kikao hicho maofisa hao wa jeshi waliwaeleza kuwa wamefika kiwandani hapo baada ya kushindwa bei ya madawati iliyotolewa na Rais ya sh.50,000 kwa kila dawati kwani gharama zao za kutengeneza dawati moja ni zaidi ya sh.78,000.

Alisema kwamba katika kikao hicho walikubaliana kiwanda hicho kipewe kazi ya kusambaza vyuma vya miguu ya madawati hayo vyenye ukubwa wa inchi 1x1-1.5 mm vikiwa vimepakwa rangi.

Maduhu alisema baada ya kukubaliana walianza kuwapa teknojia ya utengenezaji wa madawati hayo huku wakiendelea kuandika hadi waliporidhika na gharama ya kutengeneza dawati moja kwa sh.38,000 na sh.40,000 kwa teknolojia ya kiwanda hicho.

Alisema baada ya kupata teknolojia hiyo walikata mawasiliano na kila walipokuwa wakiwapigia simu walikuwa hawapokei.

Alisema kiwanda hicho kimetumia zaidi ya sh.bilioni moja kwa ajili ya utafiti wa miaka mitano kwa kutembea viwanda katika nchi 17 ili kujifunza teknolojia hiyo na kuwa wao wamekuwa wa kwanza kubuni aina mpya za madawati hapa nchini.




Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu