MARUFUKU USAFIRISHAJI WA WANYAMA HAI NJE YA NCHI KWA MIAKA 3.
Na. Aron
Msigwa - Dodoma.
Serikali imesitisha rasmi utoaji wa vibali na uuzaji wa wanyama hai
kutoka katika hifadhi za Taifa kwenda nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 3 kuanzia
Juni 25,2016.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe ametoa agizo hilo
bungeni mjini Dodoma wakati akijibu hoja na michango mbalimbali ya wabunge
iliyoelekezwa kwenye wizara hiyo wakati wa Majumuisho ya Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017 ambayo imetengewa kiasi cha
shilingi bilioni 135.7.
Prof. Maghembe ameiagiza Idara ya Wanyamapori ipange na kuweka utaratibu
mpya utakaotumika kusimamia biashara hiyo pindi itakaporejeshwa tena baada ya
kumalizika kwa muda wa zuio la Serikali la miaka 3, utakaozingatia
mazingira ya uhifadhi wa wanyama hao.
ZUIO LA USAFIRISHAJI WA WANYAMA HAI NJE YA NCHI.
Amesema kumekuwa na taarifa za baadhi ya watanzania wasio waaminifu
ambao wamekua wakijihusisha na vitendo vya kusafirisha wanyama hai waliokatazwa
kinyume cha utaratibu jambo ambalo limeisababishia Serikali ipoteze mapato
kutokana na wanyama hao.
Amesema wanyama wanaoruhusiwa kusafirishwa nje ya nchi kama nyani,
Kenge,ndege, kobe, wadudu na tumbili amesema wanyama hao wamekuwa
wakisafirishwa kinyume cha utaratibu na baadhi ya wafanyabiashara wasio
waaminifu kwa ajili ya kutumiwa na makampuni ya kimataifa kwenye shughuli za
utafiti wa kisayansi wa tiba na chanjo.
Aidha, watu na makampuni hayo yamekuwa yakinufaika binafsi kwa kupata
fedha nyingi pindi yanapofanikiwa kupata chanjo au tiba husika huku maeneo
waliokotoka yakipata fedha kidogo jambo ambalo serikali ya awamu ya tano
imeamua kulifanyia kazi.
UTALII KUSINI MWA TANZANIA NA MAENEO MENGINE.
Serikali itatekeleza miradi mbalimbali ya uboreshaji wa Utalii wa Kusini
ili kuweka mazingira wezeshi na kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikisababisha
watalii kushindwa kufika katika maeneo ya hifadhi za Taifa eneo la ukanda wa
kusini mwa Tanzania.
Baadhi ya maeneo yatakayoshughulikiwa ni gharama ya usafiri wa
ndege kwenda na kurudi katika maeneo hayo kuwa kubwa hadi kufikia Dola za
kimarekani 1800 jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa watalii hao.
Serikali imepanga kuanzisha vituo vya kuwekea mafuta ya ndege mahali
vilipo vivutio vya utalii ili kuziwezesha ndege ndogo kufika kwa urahisi na
kupata huduma ya kuongeza mafuta hivyo kupunguza gharama kwa wasafiri
wanaotembelea hifadhi za eneo hilo na ndege ambazo hulazimika kurudi jijini Dar
es salaam kupata huduma hiyo.
Aidha amesema katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali itanunua
ndege ndogo za abiria ili kuwezeha watalii kufika kwa urahisi katika maeneo ya
hifadhi za Taifa.
UTAMBUZI WA MAENEO MAPYA YA UTALII.
Serikali kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya, mikoa na Wabunge
itaanzisha mpango mpya kuviorodhesha vivutio vyote vya utalii vilivyo katika
maeneo yao ili viweze kutangazwa ipasavyo na kuongeza kuwa mara baada ya
kukamilika kwa mpango huo itaandaliwa orodha ya vivutio hivyo ili vianzwe
kutangazwa rasmi.
Katika kuimarisha shughuli za utalii nchini serikali itaweka mkazo
katika uimarishaji wa utalii wa utamaduni, uimarishaji wa maeneo ya historia na
Malikale ili kuwezesha eneo hilo kuchangia zaidi katika Pato la Taifa.
ULINZI NA USALAMA WA HIFADHI ZA TAIFA.
Prof. Maghembe ameeleza kuwa suala la ulinzi na usalama wa hifadhi zote
za Taifa liko kwa mujibu wa sheria na kubainisha kuwa serikali imeanzisha
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA) litakalochukua mbuga zote
zilizokuwa na uongozi ambazo ziko nje ya TANAPA.
Jeshi hilo litapambana kikamilifu na ujangili, kuimarisha maadili na
nidhamu ya askari wa ulinzi wa hifadhi za taifa pamoja na kushughulikia maslahi
yao na kuondoa migogoro kati ya askari na wananchi.
Amesisitiza kuwa mara baada ya Bunge la Bajeti, Wizara itakutana na
wahifadhi wakuu wote ili kuweka vigezo vya kuzingatia katika majukumu yao na
kusisitiza kuwa wahifadhi wote watakaoshindwa kwenda na kasi ya vigezo
vilivyowekwa hawatajumuishwa kwenye jeshi hilo.
Aidha, amekemea vikali vitendo vinavyofanywa na baadhi ya askari wa
hifadhi kupiga raia na kuchoma nyumba za wananchi kuwa havikubaliki na ni
kinyume cha majukumu yao.
"Nimesikiliza kwa makini michango ya wabunge na nimesikia
wafanyakazi katika hifadhi zetu wanapiga raia wanaua mifugo na kuchoma nyumba
za wananchi jambo ambalo halikubaliki, hatukuwatuma kufanya hivyo"
Amesisitiza Prof.Maghembe.
KUSHUGHULIKIA MIGOGORO YA MIPAKA MAENEO YA HIFADHI.
Serikali imesema mpaka sasa kuna migogoro ya ardhi 281, kati ya hiyo 35
ambayo ni sawa na asilimia 12.5 ni migogoro ya hifadhi na kuita Mikoa
yenye migogoro hiyo kuwa ni pamoja na Mara , Tanga na Kagera inachukua jumla ya
asilimia 50.
Aidha, amesema kuwa mkoa wa Tabora unaongoza kwa kuwa na eneo kubwa la
ardhi na unaongoza kwa kuwa na migogoro mingi ya hifadhi kwa asilimia 40.
Katika kuishughulikia migogoro hiyo Serikali imeziagiza wizara za Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maji na Umwagiliaji, TAMISEMI, Nishati na
Madini, Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira pamoja na Wizara ya Maliasili na
Utalii kushirikiana pamoja katika kutatua migogoro yote ya ardhi nchini.
UBORESHAJI WA MAENEO YA HIFADHI NA MAMLAKA ZA UHIFADHI.
Amesema katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kiasi cha shilingi bilioni 1
kimetengwa kushughulikia usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo vya kisasa
katika hifadhi ya mlima Kilimanjaro vitakavyokuwa na uwezo wa kugeuza maji taka
kuwa poda kwenye njia zote za kupandia kwenye mlima huo ili kuweka mazingira ya
mlima huo kuwa safi.
Aidha,amesema kuwa Mamlaka za hifadhi za Taifa zimeendelea kuchangia
katika maendeleo ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo ujenzi wa
madarasa, miundombinu ya barabara, utoaji wa madawati katika halmashauri
mbalimbali nchini.
|
81 more
Recent photos
Show details
|
Home »Unlabelled »
Friday, May 27, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment