Saturday, May 21, 2016

SIKU YA VIPIMO


 Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (kulia) akiangalia moja ya mashine ya kisasa inayotumika kufundishia wanafunzi wa Fani ya Mizani na Vipimo ndani ya karakana ya chuo hicho leo jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yaliyoongozwa na kauli mbiu isemayo Vipimo katika dunia inayobadilika.
Mkufunzi wa Mizani na Vipimo wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi Dar es salaam Ishigita Shunashu akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosomea fani hiyo leo jijini Dar es salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vipimo duniani.
 Baadhi ya wanafunzi wa kike wa mwaka wa kwanza katika Fani ya Mizani na Vipimo katika Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE). wakiangalia moja mashine ya kujifunzia masomo hayo iliyofungwa ndani ya Karakana ya Idara ya Vipimo na Mizani.
Mkufunzi katika Idara ya Mizani na Vipimo ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) Bi. Rabia Katula akitoa ufafanuzi kuhusu namna wanavyowajengea wanafunzi wa kuhakiki ubora wa mizani  na kushughulikia matatizo mbalimbali ya mizani.
 Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wakufunzi wa chuo hicho, Idara ya Vipimo na Mizani.
Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara kampasi ya Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosomea shahada ya mizani na Vipimo.


Na. Aron Msigwa –  Dar es salaam.

Vijana wa kitanzania wametakiwa kuchangamkia fursa za mafunzo katika fani ya vipimo na uendeshaji wa mitambo mbalimbali ili Tanzania mpya ya viwanda iweze kujengwa na wataalam wazawa kutoka ndani ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam Prof. Emanuel Mjema mara baada ya kutembelea maonesho ya mizani na vipimo kwa vitendo vitendo yaliyoandaliwa na walimu na wanafunzi wa chuo hicho yakihusisha matumizi ya vifaa na teknolojia ya kisasa  ya Mizani na Vipimo.

Amesema Tanzania inahitaji wataalamu wengi wa vipimo kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa katika sekta ya Mafuta kwenye makampuni yanayouza mafuta, mafundi wa pampu za mafuta pia kwenye mitambo ya Gesi na kuongeza kuwa mahitaji wa wataalam hao kwa sasa ni makubwa kuliko idadi ya wataalam wanaozalishwa kwa mwaka.

Ameeleza kuwa sekta ya vipimo duniani kote ni sekta mtambuka kwa kuwa inagusa maeneo mbalimbali ya maisha ya mwanadamu na huchangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwemo mazingira,teknoloji, Gesi, ubunifu ambayo yote yana vipimo vyake.

Amesema kuwa CBE kama chuo kinachofundisha fani ya Mizani na Vipimo nchini kimeungana na taasisi nyingine za elimu duniani kuadhimisha Siku ya Vipimo duniani ambayo mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu isemayo Vipimo katika ulimwengu unaobadilika kuweka msisitizo katika ufundishaji unaokwenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia yanayotokea duniani  ili kukidhi mahitaji ya soko.

Amesema Siku hiyo iliasisiwa mwaka 1870 kwa lengo la kuweka viwango kwenye upimaji wa kutumia Mita na kuongeza kuwa kuanzia wakati huo siku hiyo imekuwa ikiadhimishwa duniani kote.

Amefafanua kuwa chuo cha CBE kimedhimisha siku hiyo kwa kuwa ni chuo pekee kinachotoa taaluma ya elimu na watalaam wa Vipimo Afrika Mashariki, Kati na Kusini na kubainisha kuwa nchini Tanzania taasisi za Serikali ikiwemo Wakala ya Vipimo ambayo watalaam wake wengi wamefunzwa katika chuo hicho.

Prof. Mjema amesisitiza kuwa suala la vipimo linagusa maisha ya kila siku ya wananchi kutokana na umuhimu na kuzitaja sekta kama vile viwanda, madini na uchimbaji wa Mafuta na Gesi haziwezi kufanikiwa bila kuwa na watalaam vipimo.

Ili kuhakikisha sekta ya vipimo na Mizani katika chuo hicho inakwenda  na mabadiliko yanayotokea duniani chuo hicho kimekuwa kikibadilisha mbinu za kufundishia wanafunzi na kuandaa mitaala mipya ili kukidhi mabadiliko hayo.

Aidha, amesema wao kama watalaam wa vipimo wanasimamia na kutoa ushauri kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo kupiga vita ufungashaji wa mazao kwa kutumia vifungashio vilivyozidi maarufu kama Lumbesa ambayo vinamnyonya mkulima na kusababisha apate kiwango kisichoendana fedha na wingi wa mazao yake.

Amefafanua kuwa katika kukabiliana na changamoto  ya mabadiliko inayotokana na uvumbuzi wa Gesi na Mafuta nchini Tanzania  CBE ilianzisha mitaala ya ufundishaji wa nishati hizo kuwajengea uwezo wanafunzi wanaodahiliwa ili waweze kumiliki uchumi na kusimamia rasilimali za taifa kwa manufaa ya watanzania.

Prof. Mjema ameeleza kuwa licha ya vifaa vya kisasa vya kufundishia kupatikana gharama kubwa,chuo hicho imeendelea kufanya maboresho ya ndani kununua teknolojia mpya za kisasa zinazotumia mfumo wa digitali ili kuwawezesha wanafunzi kutumia mitambo mipya.

Amesisitiza kuwa CBE imeendelea na program mbalimbali za kuwajengea uwezo wakufunzi wake kwa kuwasomesha ndani na nje ya nchi ili waweze kutoa elimu yenye ubora na viwango vinavyokubalika.

“Ni kweli dunia imebadilika na teknolojia imebadilika sana tofauti na miaka ya nyuma, ili kuendana na mabadiliko haya tumebaresha mbinu zetu za ufundishaji ili wahitimu wetu waweze kumudu mahitaji ya soko kwa kukidhi viwango vya ndani na nje ya nchi kwa kuwa suala la vipimo halina mipaka” Amesisitiza Prof. Mjema.

Kwa upande wake Mkufunzi wa Chuo hicho Bw. Boniface Nyamweru amesema kuwa mafunzo anayoyatoa kwa wanafunzi wake yanalenga kuwajengea ujuzi na uwezo wa kubuni na kuanzisha vifaa vyao wenyewe vinavyoweza kutumika kwenye masuala ya Mizani na Vipimo.

Amesema kuwa yeye kama mtalaam wa masuala ya Mizani na Vipimo anawafundisha wanafunzi wake namna ya kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusiana na ufundi kwenye  Mizani, kufanya ukaguzi wa Mizani na Mita za kupimia vimiminika mbalimbali kama mafuta ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Mizani na vipimo nchini inapata wataalam wa kutosha wenye ujuzi.

“Mpaka sasa tunao wataalam wa ndani wazawa ambao tumewajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi , wengi wao tumewafundisha sisi hapa chuoni na wana uwezo wa kufanya ukaguzi na uhakiki wa Mizani na vifaa mbalimbali vya Vipimo katika viwango na ubora unaotakiwa” Amesisitiza.

Kuhusu matumizi ya huduma ya Mizani na vipimo nchini yanaendeshwa kwa mujibu wa sheria huku akifafanua kuwa vipimo vinavyofanyika nchini ikiwemo matumizi ya mita ya kupimia mafuta (Flow Meter) eneo la bandari ya Dar es salaam vimeruhusiwa kisheria.

Faudhia Nchila mmoja wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosomea fani ya Mizani na Vipimo katika chuo hicho amesema kuwa sekta ya Vipimo na Mizani ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kwa kuwa inagusa shughuli za kila siku za maisha ya wananchi.

Amesema vipimo vinagusa sekta ya ujenzi, maji, vifaa, teknolojia na shughuli mbalimbali za ufundi katika maeneo mbalimbali nchini huku akisisitiza kuwa mahitaji ya wataalam wa vipimo nchini kwa sasa ni makubwa kutokana na mchango wake katika maendeleo ya nchi na kutoa wito kwa vijana wengi zaidi kujiunga na masomo hayo.

Naye Dunstan Binamu mwanafunzi wa mwaka wa kwanza anayesomea masuala ya sheria katika fani ya Mizani na Vipimo akieleza mchango wa fani anayoisomea katika maendelea ya nchi amesema kuwa inalenga kulinda Haki ya mlaji katika kwa kuhakikisha masuala vipimo na mizani  yanafanyika katika viwango vilivyowekwa.



Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu