Friday, June 10, 2016

manispaa ya ilala yaka nyumba kupaka rangi

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imetoa agizo kwa wamiliki wa majengo wa Manispaa hiyo kupaka rangi majengo yaliyochakaa na kuweka taa ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao.

Agizo hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Isaya Mngurumi ambaye amesisitiza kuwa suala hilo lipo kisheria kwahiyo, wamiliki wote wa majengo wanatakiwa kutekeleza agizo hilo ili kuepuka kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria.

“Sheria ya Mipango Miji inasema kuwa majengo yote yapakwe rangi zinazoeleweka na wamiliki wote wanaombwa kufata sheria na kutekeleza agizo hilo kwa muda uliopangwa ili kuondokana na usumbufu kwa hatua zitakazochukuliwa kwa atakayekaidi agizo hili”,alisema Mngurumi.

Ameongeza kuwa sio tu sheria hiyo pekee bali Sheria ya Mazingira inahusika katika kuendeleza na kupendezesha Miji kwahiyo, zoezi la  kuweka taa na kupaka rangi majengo chakavu ni moja ya njia ya kuendeleza na kuupendezesha Mji.
Mngurumi amefafanua kuwa baada ya jengo kupakwa rangi linatakiwa kupakwa tena kila baada ya miaka miwili na kwa mwaka huu zoezi limeanza rasmi Aprili na limepangwa kuisha mwishoni mwa mwezi Juni.

Aidha, Mkurugenzi huyo ametoa rai kwa wamiliki wa makampuni mbalimbali kutopaka rangi za matangazo kwenye majengo bila kuthibitishwa na kupewa kibali na Halmashauri husika kwa kuwa kutokufanya hivyo ni kukiuka sheria za Mipango Miji.

Wamiliki wote wa majengo katika Manispaa ya Ilala wanatakiwa kupata kibali kutoka katika ofisi ya Halmashauri hiyo ili kuweza kuweka matangazo mbalimbali katika majengo yoyote yaliyopo kwenye Manispaa hiyo.

MWISHO


----
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu