Tuesday, June 21, 2016

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) chini ya mkakati wa kukuza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya ujenzi Tanzania (CoST -Tanzania) limepanga kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta hiyo ili kuondokana rushwa na kuhakikisha wananchi wanaelewa thamani halisi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya umma. Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt Leonard Chamuriho wakati wa ufunguzi wa mkutano uliowashirikisha wadau wa ujenzi kutoka nchi mbalimbali Duniani kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo. Dkt. Leonard Chamuriho amesema kuwa kikao hicho kina lengo la kuweka uwazi katika miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za wananchi ili kuondokana na rushwa zinazojitokeza katika kufanikisha miradi hiyo. "Rushwa inazungumziwa sana katika suala la ujenzi ila naomba tuzidishe uwazi katika sekta hii na kuwafanya wananchi waelewe kinachoendelea katika miradi yao hii itatutasaidia sana kupambana na rushwa, na taswira ya kuwa na rushwa katika miradi ya ujenzi haitakuwepo",alisema Dkt. Chamuriho. Dkt. Chamuriho ameongeza kuwa msimamo wa Serikali ni kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa katika miradi ya ujenzi na kuwepo kwa uwazi na uwajibikaji Kutasaidia kuondokana kabisa na suala la rushwa. Aidha, Dkt. Chamuriho amewashukuru wadau wa maendeleo wakiwemo Idara ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID), Benki ya Dunia (WB) pamoja na Serikali ya Uholanzi wanaoendelea kusaidia miradi ya ujenzi iliyo chini ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) na kutoa rai kwa wadau wengine wa maendeleo kuendelea kusaidia katika miradi mingine ya maendeleo. Kwa upande wake Mwenyekiti wa CoST -Tanzania, Kazungu Magili amesema kuwa changamoto kubwa iliyokuwepo ni kuifanya CoST-Tanzania kujitegemea kwa kutosimamiwa na taasisi yoyote na kupitia mazungumzo yaliyofanywa kati ya CoST na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ana imani kuwa yataweza kufikia muafaka na kuifanya kuwa sekta inayojitegemea kabla ya mwezi Julai mwaka 2016. MWISHO
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu