VISIMA
VINGI DAR VIMECHIMBWA BILA KUFUATA UTARATIBU.
Na
Fatma Salum- MAELEZO, Dodoma.
4/6/2016.Dar
es salaam.
Serikali
imesema kuwa visima vingi Jijini Dar es
Salaam vimechimbwa bila ya kufuata kanuni na taratibu za uchimbaji hivyo maji
yake si salama kwa matumizi ya binadamu.
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Gerson Lwenge aliyasema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake Bungeni
mjini Dodoma.
Mhe. Lwenge alibainisha kuwa katika kudhibiti
mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu uliotokea mwezi Agosti 2015 Jijini Dar es
Salaam na kuenea nchini, Serikali ilifanya uchunguzi wa sampuli za maji ya
visima 108 vya jijini humo na matokeo ya
uchunguzi huo yalionesha kuwa visima 66
maji yake si salama.
“Wizara
yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau wengine ilifanya ukaguzi na
kupima uwepo wa vimelea vya vijidudu vya ugonjwa huo katika visima vya maji
vinavyotumika jijini Dar es Salaam na sampuli za maji ya visima 108
zilichukuliwa, kati ya hivyo visima 20 vifupi na visima 46 virefu maji yake
yaligundulika kuwa si salama. Kwa ujumla visima vingi vilivyopo kwenye maeneo
ya watu vimechimbwa bila ya kufuata kanuni na taratibu.” Alisema Mhe. Lwenge.
Aidha,
Waziri Lwenge alisema kuwa Serikali pia ilifanya ukaguzi wa ubora wa maji
kwenye vyanzo vya maji katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mara, Manyara, Kagera,
Kigoma, Morogoro na Dodoma ambapo vyanzo vya maji vipatavyo 600 vilikaguliwa na
kubaini kuwa maji yaliyo salama ni chini
ya asilimia 40.
Mhe.
Lwenge alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO)
imekamilisha uandaaji wa miongozo ya utekelezaji wa Mpango wa Usalama wa Maji
(Water Safety Plan) kwa Vyombo vya Watumiaji wa Maji na Mamlaka za Maji.
“Miongozo
hiyo inakusudia kuboresha huduma za upatikanaji wa maji safi na salama kwa
Mamlaka za Maji na Vyombo vya Watumiaji wa Maji Vijijini (COWSOs) kuanzia
kwenye chanzo cha maji hadi kwa mtumiaji.” Alifafanua Mhe. Lwenge.
Kutekelezwa
kwa mpango huo kutaboresha usimamizi wa usalama wa maji katika vyombo hivyo na
kuwaepusha wananchi kutumia maji yasiyo salama pamoja na kupunguza upotevu wa
maji katika mifumo ya kusambaza maji kote nchini.
MWISHO
|
Home »Unlabelled »
Saturday, June 4, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment