BASATA WAMFUNGIA NEY WA MITEGO, ALIMWA FAINI YA SH. MILIONI 1.
Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki (Ney wa Mitego).
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungia kwa kipindi
kisichojulikana Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki
maarufu kwa jina la Nay wa Mitego hadi hapo litakapojiridhisha kwamba
ametekeleza maagizo yote aliyopewa na Baraza sambamba na yeye kubadilika
katika kubuni kazi zenye maadili na zisizo dhalilisha watu wa kada
mbalimbali.
Maagizo aliyopewa Msanii Nay ni pamoja na kulipa faini (adhabu) ya
kiasi cha Shilingi milioni 1, kufanya marekebisho ya mashairi ya wimbo
wake wa ‘Pale Kati’, kufuata sheria, kanuni na taratibu za urasmishaji
sekta ya Sanaa kwa maana ya kusajiliwa na BASATA na kuhakikisha wimbo
wake umefuata taratibu zote.
Aidha, Msanii Nay ameagizwa kuwaomba radhi watanzania kwa kutoa kazi
ya muziki yenye kuvunja maadili na kudhalilisha watu wa kada mbalimbali
hususan wanawake.
Maamuzi haya yamefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria
nambari 23 ya mwaka 1984, ikisomwa pamoja na kifungu cha 30(1)(2) na
waraka wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo wa tarehe 16/7/2009
ambayo kwa sasa inafahamika kama Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo.
Adhabu hizi zimetolewa kufuatia BASATA kufanya kikao cha pamoja na
Msanii huyu jana siku ya Jumanne tarehe 26/07/2016 kwenye Ukumbi wa
Baraza na yeye kukiri makosa na kuahidi kubadilika.
Makosa aliyosomewa na yeye kuyakiri kwa maandishi ni pamoja na;
1. Kujihusisha na shughuli za Sanaa pasipo kusajiliwa na BASATA.
2. Kutoa wimbo wa “Pale Kati” na kuupakia katika mitandao ya kijamii bila kuuleta kufanyiwa uhakiki wa maudhui yake.
3. Maudhui ya wimbo wa ‘Pale Kati’ kwa sehemu kubwa hayafai kwa
matumizi ya wazi na ni kinyume cha sheria za nchi na maadili ya
mtanzania.
Ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 16/07/2016 BASATA lilitoa taarifa kwa
umma ya kuufungia wimbo wa Pale Kati kufuatia kubeba maudhui yenye
uvunjifu mkubwa wa maadili na kupambwa na picha dhalilishi kwa wanawake.
Aidha, tarehe 12/02/2016 BASATA liliufungia wimbo wa Shika Adabu Yako
wa Msanii huyuhuyu kwa makosa yanayofanana na haya. Hivyo adhabu hii
imetolewa ili kumpa muda wa kujifunza, kujitathimi na kujirekebisha kama
kweli ana nia ya kuendelea kufanya kazi ya muziki
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA.
0 comments:
Post a Comment