Na
Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Serikali
ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kusitisha zoezi la kubadili Vyuo
vya Ufundi kuwa Vyuo Vikuu kwa nia ya kuinua vijana, kukuza na kuimarisha
mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Hayo
yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na
Watu Wenye Ulemavu. Antony Mavunde alipoalikwa kama mgeni rasmi katika mahafali
ya kwanza ya vijana waishio katika mazingira magumu yaliyofanyika katika Chuo
cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), jijini Dar es Salaam.
Mhe.
Mavunde amesema kuwa Serikali imeshaanza kuchukua hatua za awali za kuimarisha
elimu na stadi mbalimbali za ufundi nchini ambapo moja ya hatua hizo ni
kusitisha utaratibu wa kuvibadili vyuo vya ufundi kuwa vyuo vikuu na imefanya
hivyo kwa sababu ya kutambua umuhimu na mahitaji makubwa ya wataalamu
wanaohitimu katika vyuo hivyo kwenye soko la ajira.
“Serikali
itaendelea kusimamia sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ya mwaka 1994
ambapo pamoja na mambo mengine, sera hiyo inaweka msisitizo katika kuweka
mazingira na kutoa elimu ya ufundi stadi katika ngazi mbalimbali ili kuendana
na mahitaji ya mafundi sanifu nchini”, alisema Mhe. Mavunde.
Naibu
Waziri huyo ameongeza kuwa amefarijika sana kuona vijana wamepatiwa mafunzo ya
elimu ya ujasiriamali, stadi za maisha pamoja na kuunda vikundi vyao vya kuweka
na kukopa ambavyo ni muhimu sana kwa wakati huu ambao Tanzania ya Viwanda
inaandaliwa.
Pia
ametoa rai kwa wazazi wenye vijana walemavu kuhakikisha wanatoa ruhusa kwa
vijana hao kuungana na vijana wengine kushiriki katika fursa mbalimbali
zinazotokea ili nao waweze kujenga uchumi wa Taifa.
Aidha,
Mhe. Mavunde ameiomba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kujitolea kuwasaidia vijana hao kwa kuwapa elimu juu ya
Mifuko hiyo ili watambue umuhimu wa kuhifadhi fedha zao ambazo zitakuja kuwasaidia
uzeeni.
Elimu
ya vijana waishio katika mazingira magumu ni Mradi wa miaka mitatu unaofadhiliwa
na Umoja wa Jumuiya ya Nchi za Ulaya na kutekelezwa na Shirika lisilokuwa la
kiserikali la Plan International, mradi huo unagharimu kiasi cha Euro
3,874,984.53 na unatekelezwa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani,
Lindi na Mtwara.
0 comments:
Post a Comment