Wasanii nchini wahamasishwa
kuchangamkia fursa ya sanaa inayodhaminiwa na British Council.
Na. Benedict Liwenga,
WHUSM.
WASANII nchini wametakiwa kuchangamkia fursa ya kazi za sanaa
ambayo inadhaminiwa na British Council Tanzania.
Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye wakati wa Uzinduzi wa
Fursa ya Sanaa kwa Tanzania na Afrika Mashariki ambayo Mdhamini wake ni British
Council Tanzania.
Mhe. Nnauye amesema kuwa, uzinduzi wa fursa hiyo utawasaidia
wasanii nchini, Mashirika mbalimbali yakiwemo Makampuni ya ndani ya Tanzania
pamoja na Afrika Mashariki pamoja na Uingereza.
Amesema kuwa, fursa hiyo ni kubwa kwa wasanii nchini na kwa
Taifa kwa ujumla, hivyo ameipongeza British Council Tanzania kwa kuja na wazo
hilo zuri kwa manufaa ya wasanii nchini.
‘’Napenda nichukue nafasi hii kuwapongeza British Council
Tanzania kwa kuwashirikisha wasanii na Makampuni mbalimbali na kuhakikisha kuwa
fursa hizi zinamfikia kila msanii ndani ya Tanzania na kuwawezesha kushirikiana
pamoja kwenye Sekta ya Sanaa na Utamaduni ndani ya Afrika Mashariki na
Uingereza kwa ujumla’’, alisema, Mhe. Nnauye.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara yake imekuwa
ikishirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya Tanzania katika kuwawezesha
wasanii katika kukuza vipaji vyao na
kupata fursa zinazowawezesha kuitangaza nchi yao.
‘’Serikali inatambua changamoto zinazowakabili wasanii wetu
na imejikita katika kuhakikisha kuwa inatoa fursa zilizopo kwa wasanii wetu’’.
Mhe. Nnauye amesema kuwa, Serikali itaendelea kuwa mstari wa
mbele kuhakikisha kwamba inazidi kushirikiana na British Council Tanzania na
wadau mbalimbali ili kukuza vipaji vya wasanii hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Masuala ya Sanaa Kenya na Afrika Mashariki
toka British Council, Bi. Rocca Gutteridge amesema kwamba, fursa inayodhaminiwa
na British Council inalenga kuwawezesha Wasanii wa Tanzania na Afrika Mashariki
kwa ujumla kuwa karibu kwa kushirikiana katika vipaji vyao na hivyo wameanzisha
na platfomu maalum ambayo wasanii hao watakuwa wakisaidiana katika kazi zao.
Naye Kaimu Mkurugenzi British Council Tanzania, Bi. Nesia
Mahenge amesema kuwa katika kuanzishwa wa fursa hiyo, kutakuwa na Miradi kati
ya mitatu hadi tano ambayo itachaguliwa katika mwaka wa 2016/17 ambapo kila mradi utapewa fedha kiasi cha
Euro elfu 20.
Ameongeza kuwa, British Council inalenga kusaidia zaidi ya
wasanii 60 wa Afrika Mashariki ambapo wataweza kusafiri ndani ya Afrika
Mashariki kwa kipindi cha miezi tisa ijayo.
.
0 comments:
Post a Comment