Friday, October 21, 2016


Na. Judith Mhina na Lilian Lundo - MAELEZO

Serikali kupitia Mradi wa Mpango wa Kuboresha Elimu – EQUIP (Education Quality Improvement Programme) imeendelea kuboresha mfumo wa Elimu hapa nchini katika nyanja ya mitaala kwa wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka la tatu, uongozi bora katika shule za msingi pamoja na mifumo ya utoaji taarifa na takwimu sahihi.

Mratibu wa mradi huo hapa nchini Bw Johan Bentinck, amesema hayo leo jijini, Dar es Salaam alipokuwa akitoa maelezo ya utekelezaji wa  mradi huo na namna ambavyo umefanikiwa katika kuboresha Elimu  kwa wanafunzi wa shule za msingi katika mikoa saba hapa nchini.

Mradi huo umetoa fursa kwa walimu kupata mafunzo ya namna ya ufundishaji bora utakaomuwezesha mwanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu kujua kusoma, kuandika na kuhesabu ndani ya muda mfupi na kwa ufasaha.

Aidha kupitia mradi huo ufundishaji darasa la Kwanza mpaka la Nne umeboreshwa ambapo mwanafunzi anaweza kuunganisha maneno kwa kutumia sauti. Vile vile kumekuwepo na njia nyingine za kufundisha kupitia nyimbo na michezo mbalimbali kwa wanafunzi wa madarasa ya awali.

Pia mradi umewezesha kuanzishwa kwa madarasa ya awali ambayo hayakuwepo katika shule za msingi zilizoko vijijini. Wanafunzi wa madarasa hayo wamekuwa wakifundishwa na walimu wa kujitolea kwa muda wa wiki 12 na baada ya hapo hujiunga na darasa la Kwanza.

Aidha mradi huo umeleta mafanikio makubwa katika sekta ya Elimu hapa nchini ambapo kasi ya ya kutamka maandiko kwa mwanafunzi wa darasa la Kwanza mpaka la Tatu ilikuwa 21.3 mwaka 2014 na sasa ni 30.0

“Mradi huo kwa sasa unahusisha mikoa ya Dodoma, Kigoma, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Mara na Lindi huku mikoa mingine miwili ya Katavi na Singida  inategemea kuongezwa mwaka 2017,” alifafanua Bentinck.

Mwisho


Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu