Wednesday, January 4, 2017

2017 UWE MWAKA WA KULIPA KODI KWA HIARI.

017 UWE MWAKA WA KULIPA KODI KWA HIARI.
Na Beatrice Lyimo- MAELEZO
4. January, 2017
MOJA ya malengo makuu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato nchini kwa lengo la kupanua wigo katika ukusanyanyi wa kodi ili kuimarisha mfumo wa utoaji huduma kwa wananchi.
Akifungua mkutano wa Bunge la 11 la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania mwaka jana mjini Dodoma, Rais Dkt. John Pombe Magufuli alisema Serikali yake itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
Rais Magufuli alisema, Serikali yake itahakikisha kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki kwa maendeleo ya nchi. 
“Hatutasita kumchukulia hatua mtu yoyote atakayekwepa kulipa kodi, tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila mnaponunua bidhaa au huduma. Kodi ni kitu muhimu kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe” alifafanua Rais Magufuli.
Aidha, alisema kuwa Serikali yake itahakikisha kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na kuziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inapunguzia uwezo wa kuhudumia wananchi. 
 
Taarifa ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inamtaka kila Mfanyabiashara anayetumia mashine ya EFD anayekwepa kutoa risiti ni kosa la kisheria ambapo adhabu yake ni kulipa faini isiyopungua sarafu ya pointi 100 hadi pointi 150 ya thamani halisi ya fedha au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.
Aidha kwa mtu yeyote atakayeshindwa kudai au kutoa taarifa ya kukataliwa kupewa risiti au ankara ya malipo ya bidhaa au huduma atakuwa ametenda kosa na ikithibitika atatozwa faini isiyopungua sarafu ya pointi 2 na zisizozidi sarafu ya pointi 100.
 
Hata hivyo kila mfanyabiashara aliyesajiliwa na kodi ya Ongezeko la la Thamani anatakiwa kuzingatia kutumia mashine za kodi za kielektroniki (EFD).
Hivyo basi Utii wa Sheria bila shuruti  katika masuala ya kutoa na kudai risiti pindi tununuapo bidhaa ni jukumu letu sote na hivyo kupelekea ongezeko la mapato kwa maendeleo ya Taifa letu.
Aidha dira ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kuongeza mapato ya ndani kwa kuimarisha ulipaji wa kodi kwa hiari, hivyo watanzania wenzangu tushirikiane na Mamlaka hiyo katika kuongeza mapato ya ndani kwa maendeleo ya Taifa.
MWISHO
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu