OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa
licha ya Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati, Maji na Mafuta (EWURA)
kuridhia ombi la TANESCO la kupandisha bei ya umeme kuanzia Januari mosi,2017
bei ya umeme haitapanda.
Rais Dkt. Magufuli
amezungumza hayo leo Jumapili ya Januari Mosi, 2016 wakati wa Ibada katika
Kanisa la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma,Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la
Bukoba anapoanza rasmi ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Kagera.
Rais Magufuli ameshangazwa
na kitendo cha watendaji waliopandisha bei ya umeme bila hata ya kushauriana na
yeye, Makamu wa Rais,Waziri Mkuu au Waziri mwenye dhamana ya Nishati na Madini
Prof Sospeter Muhongo na hivyo kumshukuru Waziri Muhongo kwa kutengua maamuzi
hayo.
''Ninamshukuru sana Waziri
wa Nishati na Madini kwa maamuzi ya kusitisha hayo kwa hiyo umeme hakuna
kupanda bei,haiwezekani unapanga mikakati ya kujenga viwanda na hasa katika
mikakati mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme mpaka vijijini,na umeme huu unaenda
kwa watu masikini walioumbwa kwa mfano wa Mungu halafu mtu pekee kwa sababu ya
cheo chake anapandisha bei,hili haliwezekani'' Alisema Rais Dkt. Magufuli.''
Aidha, Rais Dkt Magufuli
ameendelea kuwataka watanzania katika mwaka huu mpya 2017 kuendelea kufanya
kazi kwa bidii kama maandiko matakatifu yanavyoelekeza kuwa asiyefanya kazi na
asile badala ya kulalamika kuwa fedha zimepotea.
Kwa upande wake,Askofu
Msaidizi Jimbo Katoliki la Bukoba,Askofu Methodius Kilaini,akitoa mahubiri kwa
waumini waliohudhuria ibada hiyo amempongeza Rais Dkt Magufuli kwa uongozi wake
imara,huku akisema kupungua kwa urasimu katika ofisi za umma kunatokana na
utendaji kuongezeka na kuwataka wana Kagera na Watanzania kwa ujumla
kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii na uaminifu.
Mara baada ya Ibada ya Misa
Takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba,Askofu Desderius
Rwoma,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli
aliwatakia heri ya mwaka mpya waumini wa kanisa hilo na watanzania kwa ujumla.
Jaffar
Haniu
Naibu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kagera.
01
Januari, 2017
0 comments:
Post a Comment