NEC YAONYA WANAOKIUKA
MAADILI
NA BEATRICE
LYIMO-MAELEZO
10/01/2017
Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) imevionya vyama vya siasa na wagombea wanaoshiriki katika uchaguzi
mdogo wa mbunge na madiwani kuheshimu na kuzingatia Maadili ya uchaguzi katika
kampeni zinazoendelea.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar
Hamid M. Hamid alisema kuwa vyama au wagombea watakaokiuka maadili ya Uchaguzi katika
mikutano ya kampeni inayoendelea katika maeneo yenye uchaguzi mdogo
watachukuliwa hatua.
Alisisitiza kuwa kwa
mujibu wa kipendele cha 5.3 cha maadili ya uchaguzi, chama au mgombea
atakayekiuka maadili hayo katika jimbo au kata yenye uchaguzi mdogo atafikishwa
katika kamati ya maadili ngazi husika na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu
wa kipengele cha 5.10 cha maadili ya uchaguzi ya mwaka 2015.
“Katika kampeni
zinazoendelea, baadhi ya vyama vya siasa vimeanza kukiuka taratibu za kampeni
na maadili na kutumia fursa hiyo vibaya ikiwa ni pamoja na kuwasema viongozi
vya kitaifa, kutoa matamko ambayo kihalisia siyo ya kumnadi mgombea wao,”
alisema Jaji Mst. Hamid.
“Hivyo Tume inavitaka vyama na wagombea
kuheshimu na kuzingatia maadili ya uchaguzi” alisema Mwakamu Mwenyekiti Huyo.
Aidha, Tume ya Taifa
ya Uchaguzi inatoa wito kwa wagombea na vyama vya siasa kufanya kampeni za
kistaarabu, amani na utulivu, wote wanahimizwa kuzingatia, Sheria za Uchaguzi,
Kanuni na Maadili ya Uchaguzi.
Kwa mujibu wa
kipengele cha 2.1(m) cha Maadili ya Uchhaguzi, Vyama vya Siasa, wagombea na
wafuasi wao wanatakiwa kufanya kampeni kwa kuzingatia misingi inayolenga
kutangaza Sera zao ambayo haijengi chuki, mfarakano na mgawanyiko wa jamii.
Kwa sasa vyama vya
siasa na wagombea wanashiriki kwenye kampeni za Uchaguzi Mdogo unaotarajiwa
kufanyika Januari 22 mwaka huu katika Jimbo la Dimani Zanzibar na kata 20 za
Tanzania Bara.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment