Sunday, January 8, 2017

UFUNGUZI WA SKULI YA SEKONDARI YA MOHAMED JUMA PINDUZI MKANYAGENI PEMBA

RAIS wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amesema kuwa Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 ndiyo yaliowapa uhuru wanyonge na kuwaondoshea maisha ya matabaka na kuwawezesha watoto wa wanyonge kupata elimu bure ikiwa ni miongoni mwa malengo ya Mapinduzi hao.
Dk. Shein aliyasema hayo leo  mara baada ya kuifungua skuli mpya ya Sekondari Mkanyagani, Mkoa wa Kusini Pemba  aliyoipa jina la Mohammed Juma Pindua kwa heshima kubwa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na historia yake na mchango mkubwa wa  mzee huyo katika kuifanyia kazi kubwa Serikali, hafla hiyo ni miongoni mwa shamra shamra za sherehe za Mapinduzi matukukufu ya Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa ipo haja ya kuyatunza na kuyaenzi Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kutokana na kuondosha madhila mbali mbali yaliokuwepo hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar hapo mwanzo haikutawaliwa na wananchi wake walikuwa wakijitawala wenyewe na ndipo baada ya kuja wakoloni wakaanza ukoloni sambamba na utumwa.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa historia ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 huku akiwasisitiza wazazi kuwafundisha historia vijana wao ili waijue nchi yao na wayajue Mapinduzi sambamba na kujijuwa walikotoka, walipo na wanapokwenda.
Hivyo, alisema kuwa iwapo wataijua vyema historia ya nchi yao pamoja na Mapinduzi yao ya Januari 12, 1964 hawatodanganyika wala kusikiliza kasumba za watu wachache waliokuwa hawajitambui na wanaojitoa ufahamu na kusisitiza kuwa wale wote wanaoyabeza mafanikio ya Mapinduzi basi watambue kuwa wanabeza maneno ya Mwenyezi Mungu.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuwaletea maendeleo wananchi wake wote huku akieleza namna alivyochukua juhudi katika kuhakikisha eneo hilo linapata maendeleo katika uongozi wake kabla, baada na wakati alipokuwa Mwakilishi jimbo hilo la Mkanyageni na hadi hivi leo akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua juhudi kubwa za kupeleka maendeleo katika eneo hilo lote ambalo kabla ya hapo huduma muhimu zilikuwa hazipo zikiwemo maji safi na salama, miundombinu ya barabara, umeme, vituo vya afya vya uhakika na huduma nyenginezo muhimu.
Alisema leo hii Mkanyageni imebadilika na kila mmoja anaiona na kueleza kuwa mafanikio yote hayo ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya CCM na kuwataka wananchi kuwapuza na waliofilisika kisiasa na kuyabeza maendeleo hayo wakiwemo wanaopita wakisema nchi yao imechukuliwa huku akiuliza ni nani aliyeichukua nchi hiyo.
Dk. Shein akitoa historia fupi ya elimu hapa nchini alisema kuwa Wakoloni waliacha skuli mbili tu za maandalizi, skuli za msingi zilikuwa 62 tu na skuli za Sekondari zilikuwa 4 nchi nzima ambapo hivi sasa idadi ya skuli katika ngazi ya elimu ya lazima zimefikia 843 katika mwaka 2016.
Kwa upande wa Pemba Dk. Shein alisema kuwa hadi kufikia mwaka  1963, kulikuwa na skuli 21 ikiwa ni pamoja na skuli moja tu ya Sekondari ya Fidel Castro ambayo kabla ya Mapinduzi ilikuwa ikiitwa Seyyid Abdallah, na kufikia Disemba mwaka jana skuli za Serikali zimefikia 184, ambapo skuli za Sekondari zikiwa 61 na baada ya kufunguliwa skuli hiyo mpya zitakuwa 62.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wazazi kutekeleza vyema jukumu lao la malezi, pia, aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazoikabili skuli hiyo mpya huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuiimarisha elimu ikiwa ni pamoja na kuiongezea Bajeti Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alieleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu na kupongeza uongozi wa Dk Shein katika kuiimarisha sekta hiyo na hatimae kupata mafanikio yanoyoonekana.
Mapema katika risala ya ufunguzi wa jengo hilo iliyosomwa na Maalim Salim Kuza Farhan alisema kuwa Mapinduzi yaliopelekea kutangazwa elimu bure kwa wanyonge leo yameonesha ushahidi kwa jengo hilo ambalo mtoto wa mnyonge na wa tajiri watapata elimu kwa usawa wao.
Alisema kuwa usanifu wa majengo hayo ulifanywa na Kampuni ya PSM iliyoko Dar-es-Salaam ambapo ujenzi ulianza tarehe 28.8.2012 na kufanyiwa usimajizi na washauri waelekezi kwa awamu tatu.
Aidha, alisema kuwa Mkandarasi wa ujenzi huo ni Kampuni ya kizalendo ya Rans ambapo ujenzi huo unajumuisha jengo la madarasa na utawala lenye vyumba 16 vya madarasa, vyumba 2 vya maabara, chumba cha kompyuta, maktaba jengo la dakhalia lenye vyumba 38, jengo la jiko na ukumbi wa kulia, jengo la nyumba za walimu lenye nyumba 8, ambapo ujenzi wake umegharimu TZS Bilioni 4.
Nao Wakandarasi wa Kampuni ya Rans walimueleza Dk. Shein umhimu wa Serikali kuzitumia kamuni za kizalendo ambazo zina manufaa makubwa sana huku akiomba baadhi ya vipengele vinavyowakwaza katika taratibu za tenda kuregezwa ili iwe rahisi kwao kuapata tenda za ufundi.
Viongozi mbali mbali wa Serikali, dini vyama vya siasa na wananchi walihudhuria katika hafla hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Rais a Zanzibar na Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akifungua pazia kuashiria uzinduzi wa Skuli mpya ya Sekondari Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba,iitwayo Mohamed Juma Pindua, ikiwa ni shamara shamara za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar (kushoto) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Riziki Pembe Juma. (Picha na Ikulu).
Rais a Zanzibar na Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akikata Utepe kuashiria uzinduzi wa Skuli Sekondari Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni shamara shamara za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar (kushoto) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Riziki Pembe Juma, (kulia) Mama Mwanamwema Shein,
Rais a Zanzibar na Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (katikati) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Riziki Pembe Juma pamoja na Viongozi mbali mbali walipotembelea chumba cha Kompyuta mara baada ya kuizindua Skuli Mpya ya Sekondari ya Mkanyageni,iliyopewa jina la Mohamed Juma Pindua,katika Kijiji cha Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Rais a Zanzibar na Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (katikati) akiangalia Vitabu mbali mbali wakati alipotembelea madarasa mbali mbali na maabara baada kuizindua Skuli Mpya ya Sekondari ya Mkanyageni,iliyopewa jina la Mohamed Juma Pindua, katika Kijiji cha Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar (kushoto) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Riziki Pembe Juma.
Rais a Zanzibar na Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na Mkwe Mama Mwanamwema Shein wakisalimiana na Viongozi mbali mbali wakati walipowasili katika Ufunguzi wa Skuli Mpya ya sekondari ya Mohamed Juma Pindua huko Mkanyageni Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba leo ikiwa ni shamara shamara za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Rais a Zanzibar na Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.  Ali Mohamed Shein (katikati) akitoa maelekezo kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Riziki Pembe Juma wakati alipotembelea madarasa mbali mbali na maabara baada kuizindua rasmi leo Skuli mpya ya Sekondari Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba,iliyopewa jina la Mohamed Juma Pindua, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar (kushoto).
Wananchi na Wanafunzi wa Mkanyageni na Vijiji jirani Wilaya ya Mkoani Kusini Pemba waliohudhuria katika sherehe za Ufunguzi wa Skuli Mpya ya Sekondari ya Mkanyageni, iliyopewa jina la Mohamed Juma Pindua, wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipozungumza nao leo katika shamra shamra za maadhimisho ya miaka 35 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Baadhi ya Wananchi na Wanafunzi wa Mkanyageni na Vijiji jirani Wilaya ya Mkoani Kusini Pemba wakimsikiliza Rais a Zanzibar na Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipozungumza nao leo katika uzinduzi wa Skuli ya Sekondari ya Mkanyageni,ilyopewa jina la Mohamed Juma Pindua, ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya miaka 35 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Januari 07 2017.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu