Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Mhe. George Simbachawene pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakiwa katika picha ya pamoja na wadau
mbalimbali toka Mashirika na Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi wakati wa hafla ya uchangiaji
fedha kwa ajili ya kuendeleza michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA 24 Mei, 2017
Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA BENEDICT
LIWENGA-WHUSM)
Na Husna Saidi-MAELEZO.
Katika kuendesheza michezo mbalimbali
nchini ikiwemo mashindano ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari (UMISETA) pamoja na Umoja wa Michezo ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA),
zaidi ya shilingi milioni 800 zinahitajika katika kuendesha mashindano hayo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. George
Simbachawene wakati wa hafla ya uchangishaji fedha kwa ajili ya michezo hiyo.
Waziri Simbachawene alisema kwamba, Serikali ina jukumu la
kuendesha michezo shuleni katika shule za msingi na sekondari ili kutafuta
vipaji vya vijana mbalimbali ambao wataweza kuliwakilisha Taifa na kuongeza
vipato vyao kwa manufaa yao na familia zao.
Aidha. Alisema kuwa kwa sasa Serikali inakusudia kuendesha
mashindano hayo kuanzia ngazi za shule za msingi na sekondari kwani huko ndiko
vipaji vingi vinakopatikana.
“Kuna shule mbalimbali za michezo zinaendelea kuendesha
michezo kwa wanafunzi na ndizo zinasaidia kuibua vipaji mbalimbali vya vijana,
hivyo kuna haja ya kukuza vipaji kwa vijana wetu kupitia shule wanazosoma”,
alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, baadhi ya changamoto zinazokwamisha
mashindano ya michezo ni pamoja na ufinyu wa viwanja vya mazoezi, fedha kwa
ajili ya kununulia vifaa mbalimbali vinavyotumika na wanamichezo kwani baadhi
ya vifaa hivyo vinauzwa kwa gharama kubwa.
Kwa upande wake Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amewaeleza wadau wa
michezo nchini juu ya umuhimu wa mashindano hayo ambapo amesema kwamba, kuna
haja ya kuisadia sekta ya michezo na kuthamini vipaji vya vijana nchini ili
waweze kuliletea sifa Taifa.
Dkt. Mwakyembe alisema kuna baadhi ya
vijana ambao wanavipaji vikubwa katika michezo mbalimbali hususani mpira wa
miguu, hivyo vijana hao wanatakiwa kupewa hamasa ili waweze kujituma zaidi.
“Mashindano haya ya UMISETA na
UMITASHUMTA yatasaidia kuibua vipaji mbalimbali vya vijana wetu kwani kuna
vijana wengi ambao vipaji vyao vimejificha na wanajua michezo mbalimbali”,
alisema Dkt. Mwakyembe.
Wadau
walioshiriki hafla hiyo ni 13 ambapo kati yao walitoa shilingi milioni
30 huku wadau wengine wakitoa ahadi ya kuchangia mashindano hayo.
Mashindano hayo kwa mwaka huu
yanatarajiwa kushirikisha jumla ya Mikoa 28 ya Tanzania Bara na Visiwani ambapo
kwa mara ya kwanza Tanzania Visiwani inatarajiwa kushiriki katika mashindano
hayo.
MWISHO
|
0 comments:
Post a Comment