Na Shamimu Nyaki - WHUSM.
Serikali imewataka wasanii kutengeneza kazi nzuri
zenye ubora zinazozingatia maadili ya Kitanzania ili kuwavutia wawekezaji wengi
wanaotaka kudhamini kazi hizo katika kuziandaa
na kuzisambaza.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri
wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakati
akizindua Mfumo wa MaxBurudani ulioandaliwa na Kampuni ya MaxMalipo ambapo ameishukuru
Kampuni hiyo kwa kuamua kuchukua dhamana ya kusambaza kazi za wasanii ili
kuondoa kero ya muda mrefu ya wizi wa kazi za wasanii hao kupitia njia
mbalimbali walizokuwa wanatumia wasanii hao ambazo zilikua zikiwalipa kiasi
kidogo.
“Nimefurahishwa sana na Mfumo huu namna ambavyo
utaweza kutatua changamoto ya wizi wa kazi za wasanii wetu kwa vile umeonyesha
wazi namna ambavyo msanii anaweza kunufaika na kazi yake kuanzia idadi ya kazi
zake zilizoenda sokoni,asilimia anazopata kwa kazi yake ambayo ni kuanzia 40-50
pamoja na kumuwezesha kutouza Haki Miliki yake kama walivyokuwa wanafanya hapo
awali.”Alisema Mhe.Mwakyembe.
Aidha amewataka Wasanii kutengeneza kazi zenye
ubora ambazo zitakidhi vigezo vyinavyotakiwa na Kampuni hiyo ambapo pia
ameiagiza Kampuni hiyo kutochukua kazi yeyote ambayo itakuwa haina ubora wala
kuwa na maadili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo
Mhandisi James Kasati amesema kuwa Mfumo wa MaxBurudani inalengo la kuhakikisha
wasanii wananufaika na kazi zao kwa kuwa ndio kundi lililoajiri vijana wengi
hapa nchini.
Mhandisi Kasasi ameongeza kuwa Mfumo huu utatumia
mawakala wa Max Malipo katika kusambaza kazi hizo ambapo Msanii atatakiwa
kupeleka kazi ambayo itakuwa imekidhi vigezo vya kusmbazwa na Kampuni hiyo ndani
na nje ya nchi kwa zile nchi ambazo Kampuni hiyo ina matawi.
“Mfumo huu utatumia teknolojia katika kusambaza
kazi za wasanii,kulinda Haki Miliki za Wasanii lakini pia msanii kujua takwimu
sahihi za mchanganuo wa kazi yake pamoja na namna ambavyo anaweza kulipa kodi
kwa Serikali”.Alisema Mhandisi Kisati.
Naye Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bibi.Joyce
Fissoo amesema kuwa Bodi yake inapokea Kampuni au mtu yeyote ambae anataka
kusambaza kazi za wasanii endapo tu atakuwa anawalipa Wasanii hao kile
wanachostahili kupata kupitia kazi hizo.
Aidha Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) Bw. Godfrey Muingereza mbali na kuipongeza Kampuni hiyo kwa Wazo zuri
lakini pia ameishauri kuona ambavyo inaweza kuwasadia wasanii hao kupata mikopo itakayowasaidia kuandaa na kutengeneza
kazi nzuri.
Mfumo huo tayari umeanza kupokea baadhi ya kazi za
wasanii tayari kwa kuzisambaza ambazo ni Filamu ya Kampuni ya J For Life, Albamu
ya Fiesta pamoja na Albamu ya Msanii wa
Nyimbo za Injili Bw. Godluck Gosbert.
Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akikata utepe leo Jijini Dar es Salaam kuashiria uzinduzi wa Mfumo wa MaxBurudani ulioandaliwa na Kampuni ya MaxMalipo wenye lengo la kusambaza kazi za wasanii.
Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza kulia) pamoja na viongozi wa Kampuni ya MaxMalipo wakionyesha baadhi ya kazi za wasanii zitakazosambazwa na Kampuni hiyo kupitia mfumo wa MaxBurudani leo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mfumo huo
Mkurugenzi wa Kampuni ya MaxMalipo Afrika Mhandisi James Kasati akizungumza na Wasanii (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa MaxBurudani ulioandaliwa na Kampuni hiyo wenye lengo la kusambaza kazi za wasanii
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo akizungumza leo Jijini Dar es Salaam na wasanii mbalimbali (hawapo pichani) waliojitokeza kwenye uzinduzi wa Mfumo wa MaxBurudani ulioandaliwa na Kampuni ya MaxMalipo wenye lengo la kusambaza kazi za wasanii
0 comments:
Post a Comment