Friday, December 28, 2012

JOHN MNYIKA AZUNGUMZIA MAANDAMANO YA MTWARA KUHUSU GESI ISILETWE DAR





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nitatoa kauli kamili baada ya kupata nakala ya risala iliyosomwa, hotuba zilizotolewa, ripoti za matukio tajwa na masuala ya ziada yaliyoibuliwa; katika hatua ya sasa natoa kauli ya awali kwamba:
MAANDAMANO NI MATOKEO YA UFISADI, UDHAIFU WA SERIKALI NA KUTOKUTEKELEZWA KWA WAKATI KWA MAAZIMIO YA BUNGE:
Mkutano na Maandamano ya wananchi wa Mtwara kutaka majibu toka  kuhusu manufaa ya miradi ya gesi  asili inayotoka katika maeneo yao ni matokeo ya madai ya ufisadi wa baadhi ya viongozi na udhaifu wa Serikali katika kuushirikisha umma katika michakato ya maamuzi ya  kisera na kitaasisi kuhusu rasilimali na miradi muhimu ya maendeleo.
Aidha, ni matokeo pia Bunge kutokuisimamia kikamilifu Serikali kwa niaba ya wananchi kwa mujibu wa ibara ya 63 ya katiba wakati serikali inapoacha kufafanua masuala yanayohojiwa na wabunge na inapokwepa kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu sekta ya nishati ikiwemo sekta ndogo ya gesi asili.
Iwapo Serikali ingezingatia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mwezi Julai 2011 na Julai 2012 miradi husika ya maendeleo ya gesi asili ingetekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi bila malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi katika mikoa yote inayohusika na miradi hiyo.
RAIS AHUTUBIE TAIFA KUHUSU GESI NA KUTUMIA MAMLAKA YAKE
Ili kurekebisha hali hiyo, nashauri Rais Jakaya Kikwete atumie hotuba yake kwa taifa ya mwishoni mwezi huu wa Disemba 2012 kueleza kwa umma undani wa miradi husika ya gesi asili  na manufaa yake kwa wananchi wa maeneo husika na nchi kwa ujumla; hatua ambayo alipaswa kuifanya tarehe 8 Novemba 2012 wakati wa uzinduzi wa mradi husika.
Aidha, Rais atumie mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ibara za 33, 34, 35, 36 kuagiza Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospter Muhongo, watendaji wengine wa Wizara hiyo na taasisi zake pamoja na watumishi wa umma mbalimbali wanaofanya kazi kwa niaba ya Rais katika maeneo ambayo miradi hiyo inatekelezwa kuchukua hatua ya kurekebisha udhaifu uliojitokeza na kutoa ufafanuzi kwa umma kwa kurejea pia masuala wabunge tuliyahoji kwa nyakati mbalimbali bungeni mwaka 2011 na 2012.

SERIKALI ITEKELEZE MAAZIMIO YA BUNGE KUHUSU NISHATI IKIWEMO KUREJESHA DOLA MILIONI 20.1 NA KUSHUGHULIKIA MADAI YA UFISADI
Kabla ya kufafanua kuhusu miradi iliyoanza hivi sasa, Rais au viongozi na watumishi wengine wa umma watakaozungumza kwa niaba yake waeleze mapato na manufaa ambayo wananchi wa maeneo husika na nchi kwa ujumla imepata kutoka gesi ilipoanza kuvunwa katika mikoa ya Kusini mwaka 2004 na hatua ambazo Serikali imechukua mpaka dhidi ya madai ya ufisadi wa baadhi ya viongozi katika mapato ya rasilimali hizo muhimu za taifa.
Serikali ieleze imefikia wapi katika kurejesha kiasi cha dola milioni 20.1 (zaidi ya Bilioni 30)  zilizopunjwa kifisadi katika mauzo ya gesi asili huku miradi ya maendeleo katika maeneo ambayo gesi hiyo imetoka kama Songosongo na maeneo mengine nchini ikiwa na upungufu wa fedha.
Ikumbukwe kwamba kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani nilieleza bungeni tarehe 15 Julai 2011 kuhusu tuhuma za ufisadi na ukiukwaji wa mikataba katika sekta ndogo ya gesi inaoihusu pia Kampuni ya Pan African Energy Tanzania (PAT) na kutaka kuundwa kwa kamati teule ya bunge kuchunguza suala hilo.
Badala yake Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliunda kamati ndogo ya iliyofanya uchunguzi uchunguzi wa masuala husika na taarifa kuwasilishwa bungeni mwaka 2011; hata hivyo mpaka sasa maamizio ya bunge kufuatia taarifa hiyo hayajatekelezwa kwa ukamilifu.


WAZIRI MUHONGO ATOE KWA UMMA MATOKEO YA UCHUNGUZI WA MIKATABA YA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI ASILI
Rais aagize Wizara ya Nishati na Madini iweke wazi ripoti na matokeo ya timu iliyoundwa na Waziri Muhongo kupitia upya kwa mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta na gesi asili ili udhaifu katika mikataba uliobainika mpaka sasa utumiwe na umma kutoa maoni na mapendekezo ya kuboresha sera, sheria, taasisi na mfumo mzima wa uingiaji wa mikataba kwa maslahi ya wananchi wa maeneo husika na taifa kwa ujumla.

NAENDELEA NA KUSUDIO LA KUTUMIA SHERIA KUPATA MIKATABA YA MKOPO WA DOLA BILIONI 1.225 NA YA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA GESI MTWARA MPAKA DAR ES SALAAM
Kwa upande wangu hata baada ya maandamano na mkutano wa wananchi wa Mtwara walioufanya wa tarehe 27 Disemba 2012, nitaendelea kutekeleza kusudio langu nililolieleza tarehe 26 Disemba 2012 la kutumia kifungu cha 10 cha Sheria
ya ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kutaka nakala ya mkataba wa mkopo wa masharti kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.225 (shilingi trilioni 1.86) kutoka China.
Nitataka pia nakala za mikataba wa mradi wa miundombinu ya gesi asilia ambayo itahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ujenzi wa bomba kuu la kusafirishia gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam lenye umbali wa kilometa 532.
Hii ni kwa sababu mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini haijatekeleza pendekezo nililowasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwamba kutokana na unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa sasa na baadaye Serikali ilipaswa kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika.
Aidha, naitaka Serikali irejee  mapendekezo niliyotoa bungeni na kutoa maelezo kwa umma ya sababu za bomba hilo kujengwa kutoka Mtwara mpaka Dar es salaam na kueleza kwa uwazi manufaa ya mradi huo na miradi mingine inayopaswa kutekelezwa katika mikoa ya Kusini kwa maendeleo ya wananchi husika.
Ikumbukwe kuwa tarehe 27 Julai 2012 nilieleza bungeni kuwa  pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo; Serikali inapaswa kueleza ni miradi ipi inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwemo kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa MW 300 Mtwara na MW 230 wa Somanga Fungu (Kilwa).
SPIKA AELEKEZE KAMATI MBADALA YA KUISIMAMIA SERIKALI KWA NIABA YA BUNGE KUHUSU NISHATI NA MADINI
Kwa upande mwingine, utekelezaji wa mradi huo unaendelea bila kuwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ingepaswa kuishauri na  kuisimamia Serikali hivyo ni muhimu Spika wa Bunge akachukua hatua kutokana na barua niliyomwandikia mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2012 ambayo mpaka sasa haijajibiwa.
Izingatiwe kwamba katika barua hiyo nilitoa mwito kwa Spika atumie madaraka na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati nyingine ya kudumu ya Bunge itayoshughulikia nishati na madini ikiwemo masuala ya gesi asili kwa sasa kufuatia hali tete na tata kuhusu sekta ndogo ya gesi asili nchini na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
28/12/2012
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu