Monday, January 28, 2013

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

TAARIFA KWA UMMA

WIZARA ITASHIRIKIANA NA WADAU KUTATUA MIGOGORO YA UHIFADHI WILAYANI LOLIONDO

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Khamis Kagasheki amewataka wananchi na wadau wote wanaoishi katika Wilaya ya Loliondo kushirikiana na Serikali katika mchakato wake wa kutatua migogoro ya ardhi inayohusiana na uhifadhi wilayani humo.
Waziri Kagasheki aliyasema hayo jana akiwa Loliondo katika mkutano kati yake na wawakilishi wa wananchi, Mashirika yasiyo ya Serikali, na Wawekezaji. Waziri Kagasheki alifanya ziara ya siku noja wilayani Loliondo ili kuzijua kero zilizopo kati ya wadau kuhusiana na mipaka ya hifadhi.
Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na Mbunge wa Ngorongoro Mhe Kaika Ole Telele, ilielezwa kuwa baadhi ya kero ni kuwa mapato yanayotolewa na Kampuni ya Uwindaji ya OBC kwa wananchi hayatoshi, hivyo yaongezwe.
Ilielezwa pia kuwa Kampuni ya Thompson Safaris inamiliki eneo ambalo ni vyanzo vya maji ambayo yanahitajiwa na wananchi wa vijiji vitatu vilivyoko wilayani humo, hivyo eneo hilo liwe huru kutumiwa na wadau wote.
Vilevile kulikuwa na malalamiko kutoka kijiji cha Ololosokwan kuwa wakati wa kupima mipaka na kuweka maboya eneo la kijiji hicho lilimegwa na TANAPA na Hifadhi ya Ngorongoro.
Aidha Madiwani wa Loliondo waliomba kuwa eneo ambalo linasimamiwa na Idara ya Wanyamapori libadilishwe matumizi ili lisimamiwe na wananchi kama Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori (WMA).
Baada ya kusikiliza kero za wadau Mhe Kagasheki alisema kuwa matatizo ya Loliondo yanayohusiana na uhifadhi sharti yatatuliwe, lakini utatuzi wake lazima ufuate sheria na busara. Alisema kuwa kutumia busara ni muhimu kwa kuwa kuna watu ambao wameishi katika baadhi ya maeneo yanayosemekana kuwa ni ya migogoro kwa muda wa miaka 40 hadi sasa.
Waziri Kagasheki alisema kuwa atafanya kazi kwa karibu na Mbunge wa Ngorongoro Mhe Kaika Ole Telele pamoja na wadau wengine ili muafaka uweze kufikiwa haraka iwezekanavyo.
Kwa upande mwingine, Waziri Kagasheki alizitaka Taasisi Zisizo za Serikali (NGOs) kuchangia katika kuleta muafaka badala ya kuchochea kutoelewana kati ya Serikali na Wananchi.
Pia Waziri Kagasheki aliwataka wawekezaji kuunda umoja ali waweze kujadili changamoto zilizopo na kuzitafutia uvumbuzi kwa pamoja badala ya kuwagawa wananchi. Aliwahimiza washirikiane na Halimashauri ya Wilaya na kuwa  misaada wanayotoa kwa wananchi inatakiwa iwekwe wazi.

[MWISHO]

George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA  MALIASILI NA UTALII
28 Januari 2013

Simu 0784 468047

Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu