Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Ijumaa, Septemba 20, 2013, ametunukiwa Shahada
ya Uzamivu (PHD) na Chuo Kikuu cha
Guelph katika jimbo la Ontario nchini Canada kwa kutambua mchango na uongozi
wake katika kuleta mageuzi ya kilimo katika Afrika.
Viongozi wa Chuo
hicho wanasema kuwa wamefanya uamuzi wa kumtunuku Rais Kikwete kutokana na
jitihada zake za kukabiliana na changamoto zinazokabili kilimo, jitihada zake
za kuleta usalama wa chakula na pia majaribio makubwa ya kuongeza matumizi ya
technolojia katika kilimo cha Tanzania na Afrika.
Rais Kikwete ambaye
amewasili Canada usiku wa Alhamisi, Septemba 19, 2013 akitokea Washington,
D.C., Marekani ambako alikuwa kwa siku mbili akitokea Jimbo la California amekuwa
Mtanzania wa kwanza kutunukiwa shahada ya juu kabisa katika historia ya Chuo
hicho.
Chuo cha Guelph ni
moja ya vyuo vikuu vinavyoheshimiwa zaidi katika Canada na duniani katika
Nyanja za kilimo na kilianzishwa rasmi kama Chuo cha Kilimo cha Jimbo la
Ontario Mei Mosi, mwaka 1874.
Chuo hicho ambacho
kimejipatia umaarufu kutokana na ubora wa shughuli zake za utafiti kimekuwa
katika mstari wa mbele kutafuta majawabu ya changamoto zinazoikabili dunia
katika masuala ya kilimo, raslimali za maji, matatizo makubwa ya magonjwa ya
mimea, matatizo ya ukuaji haraka wa miji duniani na changamoto za biashara za
kimataifa.
Katika miaka ya
karibuni kufuatia tishio kubwa kimataifa la ongezeko la bei za vyakula duniani
na hasa katika nchi masikini, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la uchafuzi wa
hali ya hewa, uharibifu wa mazingira, changamoto za upatikanaji wa maji safi na
salama duniani, kazi ya Chuo hicho imeongezeka sana.
Chuo hicho kimeichagua
Tanzania kama nchi ya kufanya nayo kazi katika Afrika kukabiliana na changamoto
hizo na kimemtambua Rais Kikwete kutokana na mchango wake mkubwa katika sekta
ya kilimo katika miaka yote ya uongozi wake na mipango yake ya kuboresha kilimo
katika Tanzania kama ASDP, Kilimo Kwanza na SAGCOT ambayo yote inasifiwa sana
kimataifa.
Chuo hicho kina
mahusiano ya karibu na Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam, Sokoine cha Mzumbe - Morogoro
na UDOM - Dodoma. Kati ya mwaka jana na mwaka huu, Chuo hicho kimetiliana saini
Makubaliano ya Ushirikiano (MOU) na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine cha
Mzumbe - Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Mara nne kati ya
Januari, mwaka jana, 2012 na Juni, mwaka huu, 2013, uongozi wa Chuo hicho
ukiongozwa na Rais na Makamu Mkuu wa Chuo, Dkt. Alastair Summerlee na Makamu wa
Rais wa Utafiti Dkt. Kevin Hall umetembelea Tanzania na kukutana na viongozi wa
Serikali pamoja na wale wa Vyuo Vikuu vya Dar Es Salaam na Sokoine cha Mzumbe,
Morogoro.
Mbali
na ujumbe ambao unaongozana na Rais Kikwete, sherehe za kutunukiwa kwa Kiongozi
Mkuu huyo wa Tanzania pia zimehudhuriwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa Mhe Bernard Membe, Jumuia ya Watanzania wanaoishi Canada pamoja na
maofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
20 Septemba, 2013
0 comments:
Post a Comment