TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa Tatu wa Mwaka wa Kitaifa wa Mashauriano Kati ya MCT na
Wahariri kufanyika Kilimanjaro
Baraza la Habari Tanzania (MCT) litafanya mkutano wake wa tatu wa mwaka
wa Mashauriano na Wahariri huko Machame, mkoani Kilimanjaro kuanzia Mei 29 hadi
30 mwaka huu. Mkutano huo utafunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Mheshimiwa Leonidas Gama.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga amesema huu utakuwa ni mkutano
wa tatu wa aina hii kufanyika hapa nchini, ambapo wahariri wapatao 52 kutoka
nchini kote watahudhuria.
Alisema mkutano huo umeandaliwa mahususi kuliwezesha Baraza na Wahariri
ambao ni watendaji muhimu katika vyombo vya habari, kukutana na kujadiliana
masuala muhimu yanayohusiana na taaluma na changamoto ambazo vyombo vya habari
vinakutana nazo, na hivyo kutafuta njia ya kuzipatia ufumbuzi.
Kauli mbiu ya mwaka huu inasema: “Kuimarisha
Weledi na Maadili ya Uandishi wa Habari.” Katika mkutano huo, Baraza la
Habari na Wahariri wataweza kutathimini na kuangalia changamoto ambazo
zilijitokeza toka mkutano wa pili ulipofanyika.
Mada mbali mbali
zinazotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na Ripoti ya Ufuatiliaji
wa Vyombo vya Habari ya mwaka 2013, changamoto ambazo wahariri wanakutana nazo
kwenye vyumba vya habari na Rasimu ya pili
ya Katiba mpya, Ibara ya 30 na 31.
Wahariri hao pia
watajadiliana juu ya masuala mengine muhimu ikiwemo jukumu la
vyombo vya habari katika uchaguzi mkuu ujao na changamoto zake, ripoti ya
majaji wa EJAT 2013, pamoja na ushirikiano kati ya vyombo vya habari na
serikali.
Mkutano wa pili wa mashauriano kati ya MCT na Wahariri ulifanyika mwaka jana mwezi Mei mjini Tanga na kuhudhuriwa na wahariri 45.
Mkutano wa pili wa mashauriano kati ya MCT na Wahariri ulifanyika mwaka jana mwezi Mei mjini Tanga na kuhudhuriwa na wahariri 45.
Kajubi D. Mukajanga
Katibu Mtendaji
Mei 23, 2014
0 comments:
Post a Comment