Na: Hassan Hamad, OMKR
Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ameonya kuwa vitendo vya hujuma
dhidi ya raia na wageni, vinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa
Zanzibar.
Amesema Zanzibar
ambayo imekuwa ikitegemea zaidi sekta ya Utalii kuendeleza uchumi wake na
kukuza pato la taifa, imekuwa ikiguswa na matukio hayo ya hujuma, na kwamba
yanaathiri uchumi, ustawi wa jamii na sifa ya ukarimu kwa Zanzibar.
Mhe. Maalim Seif
ametoa kauli hiyo katika mahojiano maalum na kituo cha televisheni cha ITV,
Mikocheni Dar es Salaam.
Amesema katika
kukabiliana na vitendo hivyo, serikali inakusudia kutekeleza mpango wake wa
kuweka kamera za CCTV katika maeneo muhimu ya utalii likiwemo eneo la Mji
Mkongwe, ili kuweza kuwabaini kwa urahisi wahusika wanafanya vitendo hivyo.
Kuhusu zao la karafuu
kwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar, Maalim Seif amesema serikali imefanikiwa
kudhibiti magendo ya karafuu baada ya kuongeza bei ya zao hilo na kuwashinda
wanunuzi wengine wa Afrika Mashariki ambako karafuu hizo zilikua zikipelekwa.
Aidha amesema katika
kuhakikisha kuwa ubora wa karafuu za Zanzibar unalindwa na kudhibiti wauzaji
wengine, Serikali kupitia Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, itaweka nembo
maalum “brand”, kuweza kuzitofautisha karafuu za Zanzibar na maeneo mengine.
Akizungumzia dawa za
kulevya, Maalim Seif ambaye ofisi yake ndiyo inayohusika na udhibiti wa dawa
hizo, amesema bado kuna kazi kubwa ya kudhibiti uingizaji na matumizi ya dawa
hizo kutokana na jiografia ya visiwa vya Zanzibar.
Amefahamisha kuwa
vita hiyo pia ni ngumu kutokana na uwezo mkubwa wa wafanyabiashara wa dawa hizo
ambao wanaweza kuwarubuni watendaji kwa pesa nyingi na kuacha kutekeleza wajibu
wao.
Amesema katika kupiga
vita dawa hizo, ni lazima kuwepo na mashirikiano pamoja na uadilifu miongoni
mwa watendaji, hasa wale wanaofanya kazi katika viwanja vya ndege, bandarini na
vyombo vya ulinzi.
Maalim Seif ambaye
pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF, amesema Serikali ya Umoja wa
Kitaifa GNU itaendelea kuwepo hata baada ya uchuguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa
vile suala hilo ni la kikatiba na limewekewa misingi maalum.
Kuhusu mchakato wa
katiba mpya, Maalim Seif amesema bado serikali ina jukumu la kuhakikisha kuwa
katiba mpya inapatikana, ili kuendeza ustawi wa Taifa na kukidhi mahitaji ya
wananchi.
Amesema tayari
serikali imeshatumia fedha nyingi za wananchi, na kwamba kushindwa kukamilisha
mchakato huo kwa wakati, itakuwa ni hasara kwa serikali na taifa kwa ujumla.
Hivyo
amesema hakuna budi kwa serikali kutafuta njia mbadala za mazungumzo, kuhakikisha
kuwa mchakato huo unaendelea na unafanikiwa kwa maslahi ya Taifa.
HABARI HII HAINA
PICHA. AHSANTENI WADAU.
0 comments:
Post a Comment