*KATIBU WA BUNGE MAALUM AZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI
Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis akizungumza na waandishi wa habari leo (hawapo pichani ) kuhusu kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo za Bunge jijini Dares Salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya Khamis akizungumza na waandishi wa habari leo (hawapo pichani ) kuhusu kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ndogo za Bunge jijini Dares Salaam. Picha na Magreth Kinabo - MAELEZO
****************************************
****************************************
*SITTA - BUNGE MAALUM LA KATIBA KUENDELEA
Na Winner Abraham na Rose Masaka-MAELEZO-Dar es salaam
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Samuel Sitta, amesema kuwa Mkutano wa Bunge hilo, utaendelea kama ulivyopangwa Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma.
Amesema kuwa licha ya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, kuendelea na msimamo wao wa kutaka kususia vikao vitakavyoanza mapema mwezi ujao, lakini bado kuna mambo muhimu ya kujadiliwa.
Mwenyekiti
huyo ametoa kauli hiyo leo mjini Dar es salaam, katika taarifa yake
iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahaya
Khamis wakati wa mkutano wa waandishi wa habari.
“Kamati hiyo, imeamua kupendekeza kwa Kamati ya Uongozi kwamba Bunge Maalum la Katiba liendelee kwa sababu yapo
masuala mengi muhimu ya kikatiba ambayo yanatuunganisha kama vile usawa
wa kijinsia katika nafasi za uongozi na kuikarabati Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC).
“Mambo
mengine ni kurekebisha kikatiba masuala ya Muungano,haki za
wakulima,wafugaji,wasanii na makundi mengineyo na ukomo wa vipindi vya
uongozi,”alisema Sitta katika taarifa hiyo.
Aidha aliongeza kwamba uamuazi huo, umefikiwa baada ya wajumbe wa Kamati hiyo waliohuduria ambao walikuwa zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wote, ambapo waliendelea na kikao.
Alisema hatua
ya baadhi ya wajumbe kwenda kwa wananchi na maoni yao imekuwa siyo
muafaka na si wakati wake, hivyo Bunge hilo liwajibike katika siku za
usoni kujibu upotoshwaji wowote kuhusu mchakato wa katiba kadri
unavyojitokeza.
Aliongeza kwamba Kamati hiyo, inaona kwamba
kwa kuendelea kulisusia Bunge hilo, na kupuuza wito wa jamii kupitia
makundi mbalimbali pamoja na madhehebu ya dini inatilia shaka dhamira
halisi ya viongozi wa kundi hili la wasusiaji kupuuzia juhudi zote za usuluhishi, kunazua mashaka kuhusu lengo la ususiaji kwamba pengine agenda ya viongozi hawa ni nyingine na siyo upatikanaji wa Katiba.
Alisema Kamati hiyo inarejea kwamba wajumbe hao 629
wamekabidhiwa jukumu adhimu na la kihistoria kwa niaba ya Watanzania
jukumu ambalo hutokea baada ya miongo kadhaa ya uhai wa Taifa lolote.
“ Tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ikiwa hatutafikia maridhiano yanayotuwezesha kukamilisha kazi tuliyopewa,” alisisitiza.
Mwenyekiti huyo alisema katika ngwe ya pili inayoanza mapema mwezi ujao mkutano wa Bunge hilo, uzingatie upya baadhi ya Kanuni za Bunge hilo, ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kwamba kazi ya kujadili na hatimaye inayopendekezwa inakamilika ndani ya siku 63 zilizosalia kisheria, kati ya hizo siku 60 ni za nyongeza na tatu zilizokuwa pungufu za siku 70 za awali.
Alisema
Kamati hiyo, inaendelea kutoa wito wa wajumbe waliosusia mikutano ya
Bunge hilo, kurejea katika Bunge hilo, ambalo pekee ndiyo lina uwezo wa
kisheria wa kutatua matatizo yaliyopo.
Amesema
kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 54 kifungu cha nne na tano ya Kanuni za
Bunge Maalum la Katiba, aliteua Kamati ya Mashauriano ya wajumbe
thelathini (30) kujadili matatizo yaliyojitokeza Dodoma katika mkutano
ulipita lakini wajumbe kutoka Chama cha CUF, CHADEMA na NCCR
Mageuzi,walikisusa kikao cha jana Julai 24 mwaka huu.
“Jitihada mbalimbali zilizofanywa na sekretarieti pamoja na mwenyekiti hadi asubuhi ya siku ya mkutano hazikuweza kuwashawishi wajumbe hao wasusiaji kuhudhuria kikao, alisema Sitta katika taarifa yake.
Aliitaja athari za kutoendelea na mchakato uliopangwa wa kuandaa na hatimaye kuipigia kura Katiba mpya ni pamoja na kupoteza mabilioni ya fedha za wananchi zilizokwisha tumika katika kazi, baya zaidi ni kuiweka rehani amani ya nchi yetu kwa kuukuza mno mgogoro wa katiba na kuwagawa wananchi kwa propaganda hadi uchaguzi mkuu 2015.
0 comments:
Post a Comment