MKOA WA KUSINI
UNGUJA.
Na: Hassan Hamad (OMKR).
Aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo la
Kiembesamaki Mhe. Mansour Yussuf Himid, amejiunga rasmi na chama cha wananchi
CUF.
Mhe. Mansour ambaye amewahi
kuitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushika nyadhifa mbali mbali
ikiwemo ya Waziri wa Kilimo, amechukua uamuzi huo leo kwenye mkutano wa hadhara
wa CUF uliofanyika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Baada ya kukabidhiwa kadi ya CUF na
Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, Mhe. Mansour amesema
ameamua kujiunga na CUF baada ya kubaini na kuridhika kuwa chama hicho kimebeba
matumaini mapya ya wazanzibari.
Mhe. Mansour ambaye tayari
alishateuliwa na chama hicho kuwa mshauri wa mikakati wa Katibu Mkuu wa CUF,
amechukua kadi hiyo akiwa miongoni mwa wanachama wapya 108 waliojiunga na CUF
kwenye mkutano huo.
Mapema akizungumza kwenye mkutano
huo, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, amempongeza Mhe. Mansour kwa
kuamua kujiunga na chama hicho hadharani, na kukiita kitendo hicho kuwa ni cha
kijasiri.
Akizungumzia mafanikio ya chama
hicho, Maalim Seif amesema kimepata mafanikio makubwa katika mwaka unaomalizika
wa 2014, na kutangaza maazimia mapya ya chama hicho kwa mwaka 2015.
Ametaja mafanikio yaliyopatikana
kuwa ni pamoja na kuendelea kukubalika kwa chama hicho katika pembe zote za
Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kuhusu maazimio ya Chama hicho kwa
mwaka 2015, Maalim Seif amesema kimejipanga kuhakikisha kuwa kinashinda kwa
asilimia kubwa katika uchaguzi mkuu ujao na kuweza kuongoza serikali ya umoja
wa kitaifa.
Hata hivyo amewataka wanachama
wasibetweke kutokana na mafanikio yaliyopatikana, bali waongeze nguvu
kuhakikisha kuwa malengo ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao yanafikiwa.
Ameongeza kuwa CUF pia kimejipanga
kuimarisha uchumi na kujenga Zanzibar mpya itakayokuwa ya matumaini kwa
Wazanzibari wote.
Katika hatua nyengine, Maalim Seif
ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema katika uchaguzi mkuu
ujao hatowazuia vijana kutetea haki yao iwapo watadhulumiwa.
“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010
nilifanya kazi kubwa ya kuwazuia vijana wasifanye vurugu pale hoteli ya
Bwawani. Mwanzo niliwatuma wasaidizi wangu waende kuwaondosha lakini hakuna
aliyesikia hadi nilipokwenda mwenyewe, tena waliondoka kwa shingo upande
kabisa. Kwa hivyo uchaguzi mkuu ujao sina namna yoyote ya kuwazuia vijana
kutetea haki yao”, alifafanua Maalim Seif.
Kabla ya mkutano huo Maalim Seif
alifanya ziara ya kukagua uhai wa chama hicho katika vijiji vya Michamvi,
Bwejuu, Jambiani na Paje ambako aliweka mawe ya msingi kwenye matawi ya chama
hicho, pamoja na kupandisha bendera kwenye barza ya DAY OUT ya Paje.
………………………………………………………………………………………
Mwanachama mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, baada ya kujiunga na chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja. |
. Mwanachama mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akizungumza na wanachama wenzake , baada ya kujiunga na chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja |
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja. |
. Wanachama wa CUF wakionyesha kuunga mkono uamuzi wa Mansour Yussuf Himid kujiunga rasmi na chama hicho kwenye viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja. (Picha na Salmin Said, OMKR). |
0 comments:
Post a Comment