Saturday, April 16, 2016

KANU AONDOKA NCHINI NA KUACHA MENGI YA KUJIFUNZA









Na Dotto Mwaibale
Baada ya kufanya ziara katika sehemu mbali mbali nchini toka alivyoingia tarehe 6 Aprili akitokea nchini Kenya, balozi wa Afrika wa StarTimes, Nwankwo Kanu aondoka nchini huku nyuma akiacha somo kwa wanasoka wote wa Tanzania.
Katika ziara alizofanya, Kanu kila alipopita aliwapa vijana morari ya kuweza kupambana hasa katika michezo hususani mpira wa miguu ili nao waweze kufanikiwa kupitia michezo.
Kanu aliwahamasisha vijana haswa wanaopenda mpira wa miguu kujitoa na kuupenda mchezo huo kutoka moyoni. “Mimi nimeanza kucheza mpira nikiwa sina viatu lakini niliufurahia sababu niliupenda toka moyoni”, alisema Nwankwo Kanu.
Alibainisha kuwa ili kuwa mchezaji bora wa mpira wa miguu ni lazima mchezaji uwe na vitu muhimu vya kufuata kama vile nidhamu, juhudi na heshima mchezoni.
“Nilikuwa na nidhamu, niliupenda mpira, juhudi za mazoezi na heshima pia ndiyo maana nilifanikiwa na kuchezea vilabu vikubwa duniani ikiwemo Inter Milan na Arsenal. Sasa hivi wazazi wangu wanaishi maisha mazuri.” Nwankwo Kanu, aliwapa morari vijana waliokuwa katika kituo cha michezo cha Jakaya Mrisho Kikwete kilichopo jijini Dar es Salaam.
Balozi huyo wa StarTimes katika ziara alizozifanya ndani ya siku tano nchini, alitembelea hospitali ya Muhimbili na kupita katika Wodi ya wagonjwa wa moyo na kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa na hospitali hiyo ili kuweza kuisaidia kadri awezavyo akihihusisha pia StarTimes kuangalia jinsi gani inaweza rusha matangazo ya kuelimisha kuhusiana na magonjwa mbali mbali ya moyo. Ukizangatia na yeye ana matatizo hayo ambayo yalimpelekea kuanzisha taasisi yake ya moyo, The Kanu Heart Foundation, ambayo inawasaidia watu wengi huko kwao Naijeria hivi sasa.
“Tutaangalia kwa ukaribu zaidi ni jinsi gani tutasaidiana ila mimi pia nikiwa kama balozi wa StarTimes nitafanya jitihada za lazima kuona nitasaidia kwa namna gani lakini pia StarTimes ishirikiane na nyie ili kuona mnawezaje kurusha vipindi vitakavyo elimisha umma juu ya ugonjwa huu wa moyo,” alisema Kanu.
Akitoa nasaha zake za mwisho katika hafla iliyofanyika Serena Hotel jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kabla ya kuondoka, Kanu alisema kuwa amefarijika sana kwa mapokezi aliyoyapata toka siku ya kwanza uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam na mpaka anaondoka nchini.
“Nimetembelea Uganda, Kenya lakini mapokezi niliyoyapata Tanzania ni makubwa mno, na hii si mara ya mwisho kuja Tanzania. Nimefurahi sana kwa ukarimu wenu nawaahidi kuja tena nikipata fursa hiyo.“ Alihitimisha Kanu.
Mchezaji huyo nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Naijeria na vilabu mbalimbali vikubwa vya Ulaya kama vile Ajax, Inter Milan na Arsenal ameitembelea Tanzania kama balozi wa makampuni ya StarTimes barani Afrika kwa shughuli tofauti.
Katika uwepo wake nchini Kanu ameshiriki katika shughuli kama vile;mahojiano mbalimbali na vituo vya redio na luninga; ufunguzi wa duka la jipya la StarTimes lililopo katika jingo la Mkuki Mall jijini Dar es Salaam; kutembelea taasisi ya moyo ya Jakaya Mrisho Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili; kutoa misaada mbalimbali kwa wanafunzi wenye ulemavu wa Shule ya Msingi Mbagala Majimatitu; kutembelea na kushiriki mafunzo na vijana wa kituo cha Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dar es Salaam; kushiriki chakula cha jioni cha pamoja na wadau mbalimbali wa michezo nchini pamoja na kualikwa kama mchambuzi katika mechi ya soka la Bundesliga kati ya Bayern Munich na VFB Stuttgat katika kituo cha luninga cha TBC2.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu