Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
(kulia) akiwa na kinyago cha mwanamke baada ya kuzindua mradi wa Green
Voices Tanzania. Katikati ni mfadhili wa mradi huo, Makamu wa Rais
mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandes de la Vega, na kushoto ni
Mkuu wa Wilaya Ilala, Sophia Mjema.
MAKAMU
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan,
amesema serikali itahakikisha mradi wa kutunza mazingira nchini wa Green
Voices unakuwa endelevu na kwamba ni vyema akinamama wote nchini
kushirikishwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa Green Voices Tanzania katika ukumbi
wa Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, Mhe. Samia amesema kipindi cha
miezi mitatu ambacho mradi huo umeanza kutekelezwa nchini kimeonyesha
mafanikio makubwa na kutia hamasa kwa jamii na serikali kuona umuhimu wa
kuuendeleza licha ya kwamba ufadhili wa mradi huo ulikuwa wa mwaka
mmoja tu.
Mradi
huo wa Green Voices umefadhiliwa na taasisi ya Women for Africa
Foundation inayoongozwa na makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Maria
Tereza Fernandes de la Vega Sanz (67).
“Mimi
kama kiranja wa mazingira, ninaahidi kwamba serikali itahakikisha mradi
huu unakuwa endelevu, usiishie hapa tu, na tunataka kila mkoa na hata
wilaya zote nchini wanawake washiriki kwa sababu wao ndio wanaobeba
mzigo mkubwa wa jamii huku mazingira yakiwa yanaharibiwa,” alisema.
“Tumeuzindua
mradi huu kuashiria kwamba kazi imeanza, lakini ni lazima tuhakikishe
unakuwa endelevu na usiishie hapa,” aliongeza.
Makamu
wa Rais amesema kwamba amefarijika na ongezeko la wanawake
wanaojihusisha na miradi ya utunzaji mazingira katika kipindi kifupi tu
tangu wapatiwe mafunzo nchini Hispania.
“Kutoka
wanawake 15 waliopatiwa mafunzo miezi mitatu iliyopita, leo
nimefarijika kusikia kwamba tayari hawa wamekwishawafundisha wanawake
wengine 250, haya ni mafanikio makubwa na lazima serikali iyaunge
mkono,” alisema.
Makamu
wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, na Makamu wa Rais mstaafu wa
Hispania Mama Maria Tereza, wakisikiliza maelezo ya ukaushaji wa mboga
mboga kutoka kwa Esther Muffui wa Morogoro.
Makamu
wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, na Makamu wa Rais mstaafu wa
Hispania Mama Maria Tereza, wakisikiliza maelezo ya ufugaji nyuki kutoka
kwa akinamama wa Dakawa, Morogoro.
Makamu
wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, na Makamu wa Rais mstaafu wa
Hispania Mama Maria Tereza, wakisikiliza maelezo kutoka kwa wanahabari
wanawake wanaofanya mradi wa Green Voices Tanzania.
Awali,
Mratibu wa mradi wa Green Voices Tanzania, Secelela Balisidya, alisema
kwamba, baada ya kurejea kutoka Hispania, wanawake 10 wanaofanya miradi
mbalimbali inayolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi katika mikoa
sita ya Tanzania Bara, wameweza kuwafundisha wenzao wengine 250 na kasi
yaw engine kujifunza inaendelea.
Alisema
lengo la Green Voices ni kuhakikisha wanapanua uelewa kwa wanawake na
jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira pamoja na
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, lakini wakati huo huo kuona
kwamba wanawake wanafanya miradi inayoendana na dhima hiyo pamoja na
kuwaongezea kipato.
Naye
Balozi Getrude Mongella, amesema kwamba mradi wa Green Voices na miradi
mingine ambayo inashughulikiwa katika Bara la Afrika inaonyesha
ushirikiano wa kimataifa siyo tu kwa serikali bali kwa wanawake.
Amesema ni vyema ushirikiano wa maendeleo usiachiwe tu kwa serikali, bali unaweza ukafanywa hata kwa watu binafsi.
Bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao ya muhogo.
Kuhusiana
na ushirikishwaji wa wanawake, Balozi Mongella ambaye ndiye Mwafrika wa
kwanza kuwa mwenyekiti wa Mkutano wa Dunia wa Wanawake uliofanyika
Beijing, China mwaka 1995, amesema jitihada za kwanza zilianza katika
Mkutano wa Rio de Janeiro, Brazil mwaka 1992 kuhusu mazingira na mkutano
wa maendeleo wa Cairo, Misri 1993 pamoja na ule wa Beijing, ambapo
maazimio yaliyofikiwa ni kuhakikisha wanawake wanahusishwa katika
maendeleo.
“Jambo
muhimu ni kwamba, miradi hii yote inawahusisha wanawake, na kwa hakika
wanawake ndio wenye nafasi kubwa ya kuleta maendeleo,” alisema.
Naye
Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria Tereza Fernandes de la Vega,
amewapongeza wanawake hao wa Tanzania kwa jitihada kubwa walizozionyesha
kuhusu mradi huo na kuahidi kuendelea kuwasaidia.
Alisema kwamba, mradi huo ni wa majaribio, lakini umeweza kuleta matumaini makubwa tofauti na walivyofikiria awali.
“Julai
mwaka jana wakati nilipokuja hapa Tanzania ndipo nilipata wazo la
kuleta mradi huu kwa majaribio, lakini inatia imani kubwa kuona wazo
lile tulilotaka kulijaribu leo hii limepata mwitikio mkubwa namna hii,”
alisema Maria Tereza, ambaye ndye Rais wa taasisi ya Women for Africa
Foundation.
Mama
Maria Tereza alikuwa makamu wa rais wa Hispania kati ya Aprili 18, 2004
hadi Oktoba 20, 2010, na ndiye alikuwa msemaji wa serikali ya Waziri
Mkuu Jose Luis Rodriguez Zapatero. Yeye ni mwanamke wa kwanza kushika
nafasi hiyo katika historia ya Hispania.
Brother Danny Blog (Kisima cha Hekima na Busara)
Cell: +255 - 715 - 070 109
Whatsapp: +255 - 656 - 331 974
|
|
0 comments:
Post a Comment