Bi.
Anna Salado, Mkurugenzi wa taasisi ya Women for Africa Foundation ya
Hispania, akizungumza na akinamama wa kikundi cha Green Voices katika
Kijiji cha Kitanga (hawako pichani) na kueleza jinsi alivyofurahishwa na
mafanikio yao kwenye usindikaji wa zao la muhogo.
NAIBU
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani
Jaffo, ameunga mkono jitihada za wanawake wa Kijiji cha Kitanga wilayani
Kisarawe kusindika zao la muhogo.
Jaffo,
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisarawe (CCM), amesema yuko tayari
kushirikiana na wanawake wa kijiji hicho pamoja na wilaya nzima ya
Kisarawe kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi kutokana na zao hilo.
Akizungumza
kwa njia ya simu na mshiriki kiongozi wa kikundi cha Kitanga Green
Voices, Bi. Abia Magembe, mara baada ya ziara ya ujumbe wa taasisi ya
Mfuko wa Wanawake Afrika (WAF) kijijini hapo Julai 13, 2016, Mhe. Jaffo
alimtaka kiongozi huyo kuwasiliana naye mara moja ili kuona ni namna
gani anaweza kusaidia mradi huo ambao umeanza kuonyesha matunda mazuri
kwa wanawake na jamii kwa ujumla.
Wakati
wa ziara ya ujumbe wa taasisi ya WAF kutoka Hispania, Mhe. Jaffo
hakuwepo kutokana na kutingwa na majukumu ya kazi, lakini kwa mujibu wa
Bi. Magembe, amemtaka kuwasiliana naye haraka ili kuhakikisha jitihada
za wanawake hao zinaendelezwa.
Ujumbe
wa WAF ulioongozwa na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Anna Salado kutoka
Hispania, pamoja na mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania,
Secelela Balisidya, ulijionea namna akinamama hao wanavyosindika bidhaa
mbalimbali zinazotokana na zao la muhogo kijijini hapo.
Bi. Anna Salado akicheza wakati akinamama wa Kitanga wakiimba.
Aidha,
ujumbe huo ulielezwa kwamba, mpango wa akinamama hao kwa sasa ni
kujenga viwanda vidogo kijijini hapo ili kusindika zao la muhogo ikiwa
ni hatua mojawapo ya kuunga mkono kauli ya serikali ya kuifanya Tanzania
kuwa ya viwanda.
“Kwa
kuwa serikali imekwishaahidi kwamba inataka kuona Tanzania ya viwanda
ili kuongeza ubora wa thamani ya mazao yetu pamoja na kuzalisha ajira,
sisi tumedhamiria kujenga viwanda vidogo hapa hapa kijijini ili iwe
rahisi kwa akinamama kupata malighafi na kuwasaidia wengine kujifunza,”
alisema Mama Magembe.
Mama
Magembe, ambaye ni miongoni mwa akinamama 15 waliokwenda Hispania
mapema mwaka huu kujifunza miradi mbalimbali inayolenga kutunza
mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi, alisema kwamba
kujengwa kwa viwanda vidogo kijijini hapo kutakuwa ukombozi wa jamii
nzima hasa kwa vile wilaya ya Kisarawe inalima sana muhogo, lakini
wananchi wanapunjwa na walanguzi, hivyo zao hilo kuonekana kutowakwamua
kiuchumi.
Kwa
upande wake, Bi. Anna Salado, ambaye alimwakilisha Rais wa taasisi
hiyo, Maria Tereza Fernandez de la Vega, alieleza kufurahishwa na
jitihada za wanawake hao na akaahidi kwamba, mradi huo ni miongoni mwa
miradi itakayopewa kipaumbele katika awamu ya pili.
Alisema
kwamba, imekuwa vizuri kwa wananchi wenyewe kubuni miradi
inayotekelezeka na yenye tija, na kwa namna walivyoweza kufanikiwa
katika kipindi kifupi, wana matumaini makubwa wanawake hao na wanawake
wengine nchini watafanya vizuri ikiwa watajifunza.
Aidha,
Mratibu wa Mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia, alisema
kwamba mradi wa kusindika muhogo utaikwamua jamii katika suala zima la
kukabiliana na njaa, lakini pia utawasaidia wanawake kuongeza kipato
kutokana na kuongeza mnyororo wa thamani.
“Mmefanya vizuri sana, tunawaongeza na tunaamini kwamba, katika awamu inayofuata mtafanya vizuri zaidi,” alisema.
Hata
hivyo, aliwataka wanawake wa kikundi hicho kuwa waalimu kwa wanawake
wengine kwa kuwa lengo ni kuhakikisha wanawake wote wanapata elimu na
ujuzi na wanatekeleza miradi inayoweza kuwakwamua kiuchumi na kuwaletea
maendeleo.
Mratibu
wa Mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Secelela Balisidya,
akizungumza na akimama wa Green Voices katika Kijiji cha Kitanga,
Kisarawe.
Bi.
Secelela Balisidya, ambaye ni mratibu wa Green Voices Tanzania,
aliwapongeza akinamama hao na kuwataka wasikate tamaa kwa kuwa mwanzo
umeonekana.
Aliwaasa kudumisha umoja ili kikundi hicho kiwe cha mfano na kuwahimiza kukisajili haraka ili serikali iweze kukitambua.
“Dumisheni
umoja, vikundi vingi huanza vizuri halafu vinasambaratika, tusingependa
kuona hilo linatokea kwa sababu bado kuna fursa nyingi za kuwawezesha
wanawake na umoja ndiyo nguzo muhimu,” alisema.
Bidhaa
mbalimbali zinazotokana na zao la muhogo ambazo zinazalishwa na
akinamama wa Green Voices katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe.
Zao
la muhogo lina manufaa mengi kwani mbali ya kuutafuna mbichi,
kuuchemsha au kuuchoma, kutengeneza mchanyato; unga wake hutumika kwa
ajili ya lishe, majani yake kama mboga ya kisamvu na dawa pamoja na miti
yake inapokauka hutumika kama kuni.
Lakini pia unga wa muhogo unatumika kutengeneza bidhaa nyingine kama keki, mikate, skonzi, biskuiti, sambusa, maandazi, chapati, tambi, mafuta ya lishe, sabuni ya unga, huku maganda ya mihogo hutumika kama chakula bora cha mifugo.
Aidha, muhogo ukitwangwa mbichi na kuchujwa, maji yake yake yanatoa wanga (starch) ambao hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari (sugar syrup) na pia ni lishe nzuri.
Kilimo
cha muhogo siyo tu kitasaidia kukuza pato la mkulima, lakini kinaweza
pia kuokoa mazingira pamoja na kuisaidia Tanzania kuokoa karibu Dola za
Marekani 20 milioni sawa na Shs. 42 bilioni zinazotumika kuagiza chakula
nje, jukumu ambalo kikundi cha Kitanga Green Voices kimeamua kulibeba.
Takwimu
za kilimo cha muhogo duniani zinaonyesha kuwa, Afrika ni bara la tatu
duniani kwa kuzalisha zaidi muhogo ambapo huzalishaji takriban tani
milioni 102.6 kila mwaka.
Tanzania ni nchi ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa muhogo barani Afrika baada ya Nigeria, Ghana na Kongo DRC ambapo
inaelezwa kwamba karibu ekari 670,000 za ardhi ya kilimo zinatumika
kuzalisha muhogo, zao linalochangia karibu asilimia 15 za chakula kwa
nchi nzima ambapo karibu kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini.
Mikoa
inayozalisha muhogo kwa wingi ni Mwanza, Mtwara, Lindi, Shinyanga,
Tanga, Ruvuma, Mara, Kigoma, Pwani na maeneo yote ya Zanzibar. Ukanda wa
Ziwa ni wazalishaji wakubwa zaidi ikifuatiwa na ukanda wa kusini. Mkoa wa Ruvuma huzalisha kati ya 5-10% ya uzalishaji wote Tanzania.
Muhogo ndilo zao la pili kwa kuchangia pato la taifa kwa asilimia 19 baada ya mahindi.
Taarifa
ya Shirika la Utafiti wa Viwanda na Maendeleo ya Mazao ya Chakula
Tanzania (TIRDO) inaonyesha kuwa zao la muhogo linastawi kirahisi.
Hii
ni pamoja na kuvumilia ukame na halishambuliwi na magonjwa au wadudu
wanaoathiri mazao mengine na pia muhogo unaweza kutoa mazao mengi katika
ardhi duni ambayo mazao kama mahindi hayawezi kustawi.
Kwa
mujibu wa TIRDO, muhogo ni zao la pili kuwa na wanga mwingi baada ya
viazi vitamu ambavyo vina asilimia 20 hadi 30 ya wanga na kwamba
asilimia 84 ya zao hilo hutumika kama chakula cha binadamu.
Ofisa
Mtendaji wa Kijiji cha Kitanga, Wazir Yakoub Wazir, akisalimiana na
Mkurugenzi wa taasisi ya Wanawake wa Afrika, Anna Salado.
Mratibu
wa Mradi wa Green Voices kutoka Hispania, Alicia (kushoto) na Anna
Salado wakipata msosi huku wakiwa na madafu yao wakati walipotembelea
mradi wa kusindika muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe
Julai 13, 2016.
0 comments:
Post a Comment