2


SI LA KULIKOSA

Friday, October 28, 2016

WADAU WA HABARI


Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
Dar es Salaam
28.10.2016

KATIKA kipindi cha miaka 20 wadau wa tasnia ya habari hapa nchini wamekuwa katika vuguvugu la kudai mabadiliko ya mfumo wa sheria iliyopo sasa hasa ile ya magazeti ya mwaka 1976, ambayo kwa kipindi kirefu imelalamikiwa kuwa inavibana vyombo vya habari katika kutimiza wajibu wake kwa umma.

Wadau hao wamekuwa wakiiona Sheria hiyo kuwa ni kandamizi kwa kumpa madaraka makubwa  Waziri anayesimamia tasnia ya habari katika utoaji wa adhabu dhidi ya chombo cha habari pamoja na tafsiri ya uchochezi.

Kwa kuzingatia kilio cha wadau , ukuaji wa teknolojia na mabadiliko ya mfumo wa maisha na mahitaji halisi ya jamii katika suala zima la upashanaji, ukusanyaji na usambaji wa habari, Serikali iliona ipo haja kuanzishwa kwa chombo maalum cha kusimamia maadili, maslahi, haki na wajibu wa vyombo vya habari.

Katika kutekeleza ahadi yake kwa wadau wa habari nchini, Serikali iliwasilisha Bungeni miswada miwili ya huduma ya habari na haki ya kupata habari, ambapo muswada wa upakikanaji taarifa ulisomwa, kujadiliwa na kupitishwa na Bunge ambapo unasubiri idhini ya Rais ili kuwa sheria kamili.
Tarehe Mosi Novemba mwaka huu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ninatarajia kuanza vikao vyake vya kawadia mjini Dodoma, ambapo Serikali itawasilisha Bungeni miswada mbalimbali kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa na Bunge hilo ikiwa ni utekelezaji wa wajibu wa msingi wa chombo hicho, ambao ni kutunga sheria.

Miongoni mwa miswada inayotarajia kusomwa, kujadiliwa na kupitishwa na Bunge ni pamoja na Muswada wa sheria ya huduma ya habari, ambao  mjadala wake tayari umeteka hisia za watu wa kada mbalimbali za kijamii ikiwemo wasomi, wadau wa habari na wananchi wa kawaida waliopo ndani na nje ya nchi.

Tangu muswada huo uliposomwa Bungeni kwa mara ya kwanza tarehe 19 septemba mwaka huu, wadau mbalimbali wa habari ikiwemo vyama vya taaluma ya habari, wamiliki, wahariri na waandishi wa habari wamekuwa na misimamo na mitazamo tofauti kuhusu muswada huo.

Akizungumzia muswada huo Mkurugenzi wa Habari, Hassan Abbas anasema muswada huo umekusudia kuiongezea heshima na hadhi tasnia ya habari, ili iweze kuwa taaluma kamili kama zilizo fani za udaktari, uuguzi, ufamasia, sheria na nyinginezo.

“Fani zote duniani zina chombo maalum cha usimamizi, kwa Tanzania pia tumeliona hilo, wakati umefika sasa kwa wanahabari nao waunde bodi maalum ili kuifanya tasnia ya habari kuwa taaluma yenye kuheshimika kwa jamii inayotuzungumza” alisema Abbas

Anasema kuwa maudhui ya muswada huo umezingatia mahitaji, haja, changamoto, na mazingira ya kazi yanayomkabili mwandishi wa habari wa Tanzania katika kutekeleza majukumu yake ya kazi za kila siku.

Anasema jumla ya wadau 10 wa habari waliwasilisha maoni yao kwa Serikali, na asilimia 90 ya mapendekezo yao yameingizwa katika muswada huo.

Anazitaja taasisi hizo ni pamoja na Baraza la Habari Tanzania, Jukwaa la Wahariri Tanzania, Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari, Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN) pamoja na vyama mbalimbali vya kutetea haki za kibanadamu nchini.

Kwa mujibu wa Abbas alisema muswada huo umeweka mazingira yanayomtaka Mwajiri kutoa Bima na Hifadhi ya Jamii kwa waajiriwa wake, ya kupitishwa na kusainiwa na Rais Magufuli, waandishi wa habari watakuwa na kinga maalum ya matibabu pindi wanapopata matatizo wakiwa kazini.

Anasema kuwa hivi karibuni, waandishi wa habari wamekuwa wakikabiliwa na matatizo ya kiafya ikiwemo kuugua na kifo, na hivyo wengi wao wakijikuta wakichangisha pesa kwa ajili ya kugharamia huduma za matibabu.

Akizungumzia kuhusu kifungu cha 55 cha muswada huo kinachozungumzia mamlaka ya Waziri, Abbas anasema katika kipengele hicho madaraka ya Waziri yatajitokeza pale panapokuwepo suala la dharura na linalohusu usalama wa taifa.

Anasema kuwa yapo baadhi ya matukio yanayohitaji hatua za haraka kuchuliwa na Serikali, ikiwemo uchapishaji na utangazaji wa habari zinazohamasisha uasi, uchochezi, vurugu, mapigano ya kikoo na kadhalika ambapo Waziri mwenye dhamana ya atawajibika kukifungia chombo hicho mara moja.

Anaongeza kuwa muswada huo umetoa fursa kwa chombo na mwandishi wa habari kuikosoa Serikali kuhusu sera, miongozo, matamko na maagizo mbalimbali ya Viongozi ambayo yameshindwa kutekelezwa na Serikali.

Mkurugenzi huyo anafafanua kuwa katika mikataba na sheria mbalimbali za kimataifa ikiwemo kifungu cha 19 mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia, kimeainisha mipaka na ukomo wa waandishi wa habari ikiwemo habari zinazohusu ulinzi na usalama wa taifa, kashfa na maadili ya taifa.

Kwa mujibu wa Abbas alitoa ufafanuzi kuhusu sheria hiyo kuwabana wamiliki na watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa kuwataka kujisajili na suala hilo si la kweli kwani litahusu vyombo vya habari vilivyo katika mfumo wa machapisho ikiwemo magazeti na majarida.

“Sheria itasimamia wote wa waandishi wa habari wa magazeti, redio na televisheni suala la usimamizi wa maudhui ya vyombo vya habari vilivyopo katika mfumo wa kieletroniki ikiwemo televisheni na redio wataendelea kusimamiwa na mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA)” alisema Abbas.

Abbas anasema kuwa muswada huo umekusudia kuanzishwa kwa Bodi huru ya habari inayosimamia maadili na maslahi ya waandishi, ambapo itakuwa na wajumbe 7 na wajumbe 4 wa Baraza hilo watatoka katika tansia ya habari akiwemo Mwenyekiti wa bodi hiyo.

Aliyataka majukumu ya bodi hiyo ni pamoja na kuandaa miongozo na miiko ya mwandishi wa habari pamoja na kuandaa makongamano na mikutano ya mara itayowawezesha wadau wa habari kukutana na kujadili changamoto mbalimbali zinaoikabili tansia ya habari.

“Tasnia ya habari ni nyeti sana, hivyo ni lazima iundiwe bodi yake, bila ya bodi inaweza kuhatarisha usalama wa nchi” alisema Abbas.

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party, Augustino Mrema anasema muswada wa huduma ya habari umekuja kwa wakati mwafaka kwani tasnia ya habari nchini wamekuwa wakikabiliwa na kanzi kinzani mbalimbali ukosefu wa hifadhi ya jamii na bima ya afya.

Akizungumzia kuhusu Mamlaka ya Waziri yaliyoanishwa katika muswada huo, Mrema anasema msimamizi wa sheria ya nchi yeyote duniani ni Serikali, ambapo hata hivyo katika muswada huo Waziri amepewa mamlaka katika masuala ya dharura na usalama wa taifa.

Mrema anasema wadau wa habari ikiwemo vyama vya taaluma na wasomi kuacha malumbano yanayoendelea katika mitandao ya kijamii na badala yake waungane na kuwa wamoja ili muswada huo upitishwe na Bunge ili ipatikane sheria kamili inayowasaidia waandishi wa habari katika kipindi cha miaka 50 hadi 100 ijayo.

Naye Mhariri Mkuu wa kituo cha Redio Times, Zouhra Malisa anasema zipo taarifa zilizoenea katika mitandao ya kijamii kuhusu kigezo na sifa ya mwanahabari ambayo inamtaka mtumishi wa tasnia hiyo kuwa na shahada ya uandishi wa habari, na hivyo kuibua woga kwa mustakabali wa tasnia ya habari nchini.

Anasema kuwa kituo chake kimepanga kuwasilisha maoni kuhusu muswada huo, ambapo bodi ya wakurugenzi na uhariri ya redio hiyo imepanga kuwasilisha mapendekezo yao kuhusu muswada huo kabla ya kumalizika kwa muda uliotolewa na kamati ya kudumu ya maendeleo ya jamii ya Bunge.

Aidha Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Majira, Imma Mbughuni muswada huo ni mzuri, hususani katika kipengele cha uanzishaji wa bodi ya ithibati itayohusika katika utoaji wa vitambulisho vya wanahabari, ambavyo kwa kipindi kirefu vimekuwa vikileta usumbufu mkubwa kwa waandishi wa habari.

Aidha Mbughuni aliishauri Serikali kuusambaza huo muswada kwa wananchi wa kawaida kwa kuwa itasaidia kupunguza minong’ono na malalamiko yanayotolewa na wadau wa habari katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Jambo Leo, Anicetus Mwesa alisema uundaji wa bodi mbalimbali ikiwemo bodi ya ithibati itazidi kuijengea hadhi tasnia ya habari nchini kwani kwa kipindi kirefu wadau wa habari wamekuwa wakipendekeza vitambulisho hivyo vitolewe kila baada ya miaka mitatu baada ya utaratibu wa sasa wa mwaka mmoja.
Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu