2


SI LA KULIKOSA

Tuesday, November 22, 2016


Mzazi Sakina Lembo
TAARIFA KUHUSU MZAZI KUZUILIWA KUONDOKA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI

Kuna taarifa zimezagaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili imemzuia mzazi Bi. Sakina Mohammed Lembo kuondoka baada ya kuhudumiwa mpaka alipe kiasi cha shilingi 338,257. Taarifa hizo siyo za kweli mama huyo ameruhusiwa kwenda nyumbani na hajalipa kiasi chochote cha fedha.

Ukweli ni kwamba Hospitali ilikuwa ikikumbana na changamoto ya upungufu wa dawa na vitendanishi vya kuwahudumia akina mama hawa kwani mara nyingi vilikuwa havitoshelezi mahitaji kutokana na wingi wa wagonjwa. Kutokana na tatizo hilo Hospitali iliamua kuanzisha mfuko maalumu wa dawa (drug revolving fund) kwa ajili ya kuwahudumia akina mama wajawazito kwa lengo la kuhakikisha hakuna mama mjamzito anayekosa dawa na huduma nyingine kwa wakati. 

Ili kuhakikisha mfuko huu unadumu na kuwa endelevu kwa ajili ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vya kuwahudumia kina mama wanaofika katika hospitali kupata msaada wa kujifungua, Hospitali ilianzisha utaratibu wa kuwaomba akina mama wanaopewa huduma hizi kuchangia kadiri inavyowezekana. 

Utaratibu huu unawezesha akina mama kuhudumiwa na kupata dawa zote na vifaa vyote vinavyohitajika kwa wakati na bila bugudha ya kuwataka kwenda kununua nje ya Hospitali kabla ya kuhudumiwa. Kauli mbiu ya Hospitali ni kuwa mama akifika tu anahudumiwa kwanza na uchangiaji unakuja baadaye. Kumekuwa na mwitikio mzuri wa kuchangia kwenye mfuko huu kulingana na uwezo alionao mgonjwa husika. 

Ili kuhakikisha kwamba utaratibu huu unaendana na sera ya msamaha, akina mama wanaoshindwa kuchangia mfuko huu wamekuwa wakisamehewa kupitia utaratibu wa msamaha wa Hospitali unaoratibiwa na idara yetu ya ustawi wa jamii. Kwa hiyo hakuna mama anayezuiliwa kuondoka Hospitali kwa sababu ameshindwa kuchangia. 

Ieleweke kwamba Hospitali inatumia mfumo wa kieletroniki ambao lazima uoneshe gharama halisi aliyotumia mgonjwa yeyote. Kwa utaratibu huu, mgonjwa halazimishwi kulipia bali ni hiari na ambao hawana uwezo wanapewa huduma zote bure. Mfumo huu unafanya kazi vizuri na toka uanze akina mama wengi wamefurahishwa na huduma zetu na wamekuwa mashuhuda juu ya ubora wa huduma hii. Kutokana na utaratibu huu hakuna jinsi mama yeyote atazuiliwa kwa sababu ya kushindwa kuchangia huduma.

Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/2017, Hospitali iliwahudumia akina mama wajawazito 13,322. Miongoni mwao, akina mama waliokuja kutokea Hospitali za umma walikuwa 7,055 sawa na asilimia 53. Aidha gharama halisi za kuwapa huduma akina mama wenye rufaa 7,055 ilikuwa Tshs. 620.4 milioni. Akina mama waliweza kuchangia Tshs. 250.5 milioni. Kwa hiyo Tshs. 370 milioni sawa na asilimia 60 ziligharimiwa na Hospitali. Kuanzia mwezi Novemba mosi 2016  hadi Leo Novemba 21,2016 Hospitali imetoa msamaha kwa kina mama yenye jumla ya shilingi milioni 198.

Imetolewa na;
Aminiel Aligaesha,
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma,
Hospitali ya Taifa Muhimbili,

Novemba 21, 2016

Na Dotto Mwaibale

MZAZI Sakina Lembo (26) mkazi wa Mbagala Kibonde Maji ambaye alizuiliwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  (MNH), kutokana na deni la sh. 338,257 baada ya kufanyiwa oparesheni ya uzazi uongozi wa hospitali hiyo umemruhusu kuondoka bila ya masharti yoyote.

Akizungumza wakati akitoka hospitali hapo baada ya kuruhusiwa mama yake na Sakina, Edith Chausa alisema analishukuru gazeti la Jambo Leo kwa kutaoa taarifa hiyo ambapo wahusika wameona na kuchukua uamuzi wa kumruhusu binti yake kuondoka hospitali na mtoto wake bila ya masharti yoyote" alisema Chausa.

Alisema kabla ya kuchukua uamuzi wa kwenda kwenye vyombo vya habari waliomba kuondoka na mzazi huyo lakini walikataliwa kwa kuambia mpaka alipe deni hilo ambalo hawakuwa na uwezo wa kulipa.

"Baada ya kutoka taarifa hii kwenye vyombo vya habari amekuja wodini mkurugenzi wa Muhimbili na kuchukua maelezo kwa binti yangu huku akilalamika kuwa mbona hatukusema kama hatukuwa na fedha badala yake tumewashitaki kwenye vyombo vya habari" alisema Chausa.

Chausa alisema binti yake na mtoto waliruhusiwa kuondoka hospitali hapo saa saba mchana na kuwa hali ya mtoto na mama yake inaendelea vizuri.

Chausa ameiomba serikali kuangalia suala zima la wakina mama wanokwenda kujifungua kulipishwa kiasi kikubwa cha fedha kwani wengi wao hawana uwezo huo.

Share this article :

0 comments:

Post a Comment

 
MZUKA BLOG © Copyright 2014. All Rights Reserved.

Powered by MATERU FROM IBS.
imagem-logoRudi Juu