Wananchi wakiangalia daladala lenye
namba za usajili T 161 CRP lililoacha njia na kupinduka Mbagala Misheni
kwa Bluda Dar es Salaam leo asubuhi na kujeruhi watu watatu.
Daladala likiwa mtaroni.
Na Dotto Mwaibale
WAtu watatu wamejeruhiwa vibaya baada
ya daladala walikuwa wamepanda kutoka Temeke kwenda Mbagala Kuu kuacha
njia na kupinduka jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mtandao wa Dar es Salaam
leo asubuhi askari wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa kipolisi wa
Temeke ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji wa polisi
alisema ajali hiyo imetokea majira ya saa 12 na nusu asubuhi.
Alisema daladala hilo liliacha njia na
kutumbukia kwenye mtaro eneo la Mbagala Misheni kwa Bluda baada ya
kuteleza kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha.
Alisema baada ya ajali hiyo wananchi walifika kutoa msaada kwa majeruhi ambao walikimbizwa Hospitali ya Temeke kwa matibabu.
Alitaja daladala hilo kuwa ni lenye
namba za usajili T 161 CRP ambapo alitoa mwito kwa madereva kuwa
waangalifu wanapoendesha magari yao hasa katika kipindi ambacho mvua
zinanyesha.
Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Temeke, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP), Gilles Muroto ili
kuzungumzia ajali hiyo zilishindikana baada ya kupigiwa simu ambayo
ilikuwa ikiita pasipo kupokelewa.
0 comments:
Post a Comment