Mwenyekiti wa Chama cha Wahudumu wa Baa
Tanzania (Chawabata), Ali Hussein (kulia), akizungumza na waandishi wa
habari Dar es Salaam jana, wakati akipinga zoezi linalofanywa na
Manispaa ya Ilala la kukagua leseni za wauza vileo usiku. Kushoto ni
Katibu wa chama hicho, Boniface Lameck.
Katibu wa chama hicho, Boniface Lameck akitoa ufafanuzi
katika mkutano huo.
Na Dotto Mwaibale
CHAMA cha Wahudumu wa Baa Tanzania
(Chawabata) kimepinga zoezi linalofanywa na Manispaa ya Ilala la kukagua
leseni za wauza vileo usiku.
Akizungumza Dar es Salaam jana
Mwenyekiti wa chama hicho, Ali Hussein alisema zoezi hilo linawatisha
wateja wanapokuwa wakipata vinywaji katika baa mbalimbali.
Hussein alisema chama hicho kimepokea malalamiko kutoka kwa wamiliki wa baa ambao ni wanachama wao.
Alisema wiki moja kabla ya kuanza kwa
sikukuu za mwishoni mwaka maofisa biashara wa Manispaa ya Ilala walikuwa
wakipita katika baa mbalimbali maeneo ya Ukonga na vitongoji vyake
kuanzia saa mbili usiku kukagua leseni.
Alisema maofisa hao walikuwa wameongoza na askari polisi waliokuwa na bunduki jambo ambalo kiusalama sio zuri.
"Huu utaratibu wa kukagua leseni usiku
na mtutu wa bunduki unaweza kutoa fursa kwa wahalifu nao kwenda kwenye
mabaa na kujifanya ni maofisa biashara na kufanya uporaji tunaomba
serikali kuliangalia jambo hili" alisema Hussein.
Alisema hali hiyo imejitokeza baada ya
serikali kuzuia baa kufunguliwa asubuhi kama ilivyokuwa awali ambapo
chama hicho oktoba mwaka jana kiliiomba serikali kupitia mtandao huu na
katika vyombo vya habari kuruhusu kufunguliwa kwa baa wakati wote ili
kutoa nafasi ya wauza vileo kufanya biashara na kuweza kukusanya fedha
za kulipa kodi ya serikali.
Alisema kwa nyakati za mchana ni vigumu
kukuta baa zikiwa wazi na ndio maana maofisa hao wameamua kwenda usiku
kukagua leseni hizo jambo ambalo ni hatari kwa wateja na maofisa hao
"Muda wa kufungua baa kuanzia saa 10
jioni unawaathiri wateja wetu kwani kwa masaa matano ya kufanyabiashara
ya vileo na vinywaji vingine ni mchache mno" alisema Hussein.
Alisema hatua hiyo ya serikali ya
kuamuru baa kufunguliwa kuanzia saa 10 imeathiri wahudumu wa baa ambao
wengi wao wamepunguzwa kazi ambapo wanaiomba serikali kuangalia jambo
hilo.
Meneja wa Baa ya Serengeti iliyopo eneo
la mabaa Banana katika manispaa hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la
Emanuel alisema kitendo cha maofisa hao kukagua leseni za biashara usiku
ni kigeni kwao na kinawatisha wateja wao ambapo ameomba manispaa
kuangalia upya muda wa kufanya ukaguzi huo.
Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala,
Neema Njau alisema zoezi hilo lipo kisheria na linafanywa na kamati
maalumu iliundwa na manispaa hiyo ambayo ipo chini ya wakuu wa polisi wa
wilaya hiyo.
"Ukaguzi wa leseni hizo hauwezi
kufanyika mchana kwa kuwa baa nyingi zinakuwa zimefungwa lakini
wasiliana na ofisa biashara wa manispaa atakupa maelezo mazuri zaidi"
alisema Njau.
0 comments:
Post a Comment