Na
Ismail Ngayonga
MAELEZO
Zanzibar
10.01.2017
SERIKALI ya China
imeisifu Tanzania kwa kuzingatia sera ya uwazi katika ushindanishaji wa zabuni za
miradi ya ujenzi, ikilinganishwa na nchi nyingine zilizopo katika ukanda
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hayo yamesemwa leo
Mjini hapa na Mwenyekiti wa kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya CRJE ya nchini
China, Bw. Hu Bo wakati akizungumza na
waandishi wa habari wa Kituo cha
Televisheni ya Taifa ya nchi hiyo (CCTV) waliofika nchini kujionea miradi mbalimbali
inayotekelezwa na Serikali ya nchi hiyo Tanzania.
Hu Bo alisema
Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Barani Afrika zinazoongoza kwa kufuata
kanuni, sheria na taratibu za zabuni za ujenzi, ambapo Serikali imekuwa ikitoa
kipaumbele kwa makampuni ya ukandarasi yanayomilikiwa na wazawa na kukubali maombi
yao ya zabuni za ujenzi.
“CRJE tunafanya
shughuli zetu katika mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki ikiwemo Kenya,
Uganda, Burundi na Rwanda, katika sehemu zote Tanzania imekuwa nchi bora zaidi kwani pamoja na mazingira
salama ya kazi zetu lakini pia wakandarasi wazawa wamekuwa wakipewa nafasi
katika miradi ya ujenzi” alisema Hu Bo.
Kwa mujibu wa Hu Bo
alisema tangu mwaka 1977 kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya
ujenzi nchini, ambapo mbali na mazingira
bora ya uwekezaji yaliyopo nchini lakini pia kunatokana ushirikiano na uhusiano
wa kirafiki uliopo baina ya Serikali ya China na Tanzania.
Aliitaja baadhi
ya miradi ya ujenzi ya Serikali
iliyotekelezwa kampuni hiyo nchini ni pamoja na ujenzi wa ukumbi wa Bunge
Dodoma, Jengo la Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais Zanzibar, Jengo la Ofisi ya Wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar, Ofisi
za Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).
Aidha Hu Bo alisema
kampuni hiyo pia imekamilisha ujenzi wa majengo ya hoteli mbalimbali za kitalii
ikiwemo hoteli za kulala wageni za Melia, Tembo, Packyard, Residence, zilizopo
Zanzibar pamoja na Ujenzi wa hoteli ya
nyota tano Jijini Mwanza, Hyatt Regency ya Mjini Arusha na Ujenzi wa Daraja la Nyerere,
lililopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa
kampuni hiyo imeendelea kuaminiwa na Serikali na mashirika ya kimataifa
kutokana na kuzingatia ubora wa kazi, muda na thamani ya pesa, hivyo aliwataka
wakandarasi wa makapuni ya Tanzania kuzingatia vigezo hivyo pindi wanapopewa
zabuni za ujenzi wa miradi mbalimbali.
“Kutokana na
mafanikio makubwa yaliyofanywa na CRJE, tulishinda tuzo ya kampuni bora ya
ukandarasi kutoka nje kwa 2009, 2012 na 2015 katika Tanzania, hii imetupa
heshima na kutufanya kuongeza viwango vya ubora katika miradi ya ujenzi
tunayoisimamia” alisema Huo Bo.
Alisema Serikali ya
China itaendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano ili kuhakikisha kuwa
miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na Serikali ya China inakamilika kwa
wakati na kuzingatia ubora uliowekwa.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment