Kaimu Kamishna Mkuu TRA, Mary Maganga.
Katika kuhakikisha inaboresha huduma kwa
wafanyabiashara ambao wanaingiza mizigo nchini kwa njia ya bandari,
mipaka na viwanja vya ndege, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato nchini
(TRA) imeeleza mpango wa Serikali wa kuanza kutumia mfumo wa Dirisha
Moja la Huduma (Electronic Single Window System) ambao kwa hakika
utamaliza tatizo la mizigo kukaa muda mrefu kwa sababu ya kukosekana
vibali.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya
kumalizika mafunzo ya siku moja kuhusu mfumo wa Dirisha Moja la Huduma
kwa taasisi zinazotoa vibali na wafanyabiashara, Meneja Mfumo wa
Kieletroniki wa Dirisha Moja la Huduma, Tinka Felix alisema lengo la
kuanza kutumia mfumo huo ni kuboresha huduma ambazo wanazitumia sasa ili
wafanyabiashara wanaoingiza mizigo nchini waweze kuipata kwa haraka
kuliko ilivyo sasa.
Meneja
Mfumo wa Kieletroniki wa Dirisha Moja la Huduma, Tinka Felix
akizungumza kuhusu mfumo wa Dirisha Moja la Huduma (Electronic Single
Window System). (Picha zote na Rabi Hume - MO DEWJI BLOG)
“Ni mpango wa Serikali kuboresha huduma
kwa wateja kwa kupunguza muda wa kutoa mizigo bandarini au mipakani au
kwenye viwanja vya ndege, kupitia mfumo huu wateja hawatakuwa wakienda
kwenye idara na taasisi za Serikali na badala yake wakiwa hukohuko
kwenye ofisi zao wataweza kuomba na kupata vibali na kupata bili za
malizo kwenda kulipa benki, mfumo pia utafanya kazi na benki," alisema Felix.
Alisema Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza
kutumia mfumo huo na mataifa mengi yanautumia ili kurahisisha huduma
kutolewa kwa haraka kwani mfumo wa sasa wa forodha (tancis system)
unashindwa kufanya kazi kwa haraka jambo ambalo linasababisha mizigo
kuchelewa kutolewa kutokana na muda mrefu mmiliki kutumia kutafuta
vibali.
Mkurugenzi
wa Sera Utafiti Na Ushauri wa TPSF, Gili Teri akizungumza faida za
kutumia mfumo wa Dirisha Moja la Huduma (Electronic Single Window
System).
“Mfumo wa sasa ili mtu apate kibali
anatakiwa atembelee hizo ofisi hata mara 10 na baadhi ya ofisi wanataka
vibali zaidi ya kimoja lakini mfumo huu wa sasa muda ambao unatumika
kuomba vibali utapungua na tunategemea kuokoa Dola milioni 65 kwa
kutumia tu mfumo wa electronic single window system,” alisema Felix.
Alisema kwa sasa kuna taasisi za Serikali 47
ambazo zinatoa vibali lakini mfumo wa Dirisha Moja la Huduma utatumiwa
na taasisi 32 ambazo kwa pamoja zitakuwa zikitoa vibali 106.
Aidha alisema Serikali imeagiza kuwa mfumo
huo uanze kutumika baada ya mwaka mmoja hivyo wanategemea kuanzia
mwakani mfumo ambao watakuwa wakitumia utakuwa ni wa Dirisha Moja la
Huduma (Electronic Single Window System) ambao utawezesha
wafanyabiashara ambao wanatoa mizigo kupitia bandari, mipaka au viwanja
vya ndege kupata vibali kwa haraka.
Na Rabi Hume, MO DEWJI BLOG
Baadhi
ya washiriki wa semina hiyo ya siku moja wakiuliza maswali na kutoa
maoni kuhusu mfumo wa Dirisha Moja la Huduma (Electronic Single Window
System).
0 comments:
Post a Comment