Na
Christina R. Mwangosi, MOHA
Jeshi la Magereza nchini ni
moja kati ya Majeshi yaliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi yenye
jukumu kubwa la msingi la kuwarekebishwa wafungwa wanaohukumiwa kwa makosa
mbalimbali hapa nchini.
Katika taratibu za
Urekebishaji wa wafungwa zipo stadi mbalimbali za kilimo, ufundi na uzalishaji
ambazo zinatumika kuwarekebisha wafungwa ili hata pale wanapomaliza vifungo
vyao na kurudi uraiani waweze kutumia ujuzi walioupata katika shughuli za
uzalishaji na hivyo kujiletea maendeleo yao binafsi lakini kuchangia pia katika
maendeleo ya nchi yetu.
Mbali na jukumu hilo la
msingi la Jeshi hilo, pia Jeshi hili limekuwa likijishughulisha na shughuli
mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo shughuli za kilimo kwa ajili ya chakula
kwa wafungwa, utengenezaji wa samani mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya ofisi
na nyumbani, pamoja na utengenezaji wa viatu shughuli zinazofanyika katika
Magereza yaliyopo hapa nchini.
Aidha Jeshi la Magereza
nchini lina fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuwa na mchango mkubwa sana katika kukuza
uchumi wa nchi yetu na hivyo kufikia malengo yetu ya kuwa na uchumi wa viwanda.
Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na ardhi nyingi yenye rutuba inayofaa
kutumika kwa kushughuli za kilimo na matumizi mengineyo ya uzalishaji vikiwemo
viwanda.
Kwa muda mrefu sasa jeshi la
Magereza limekuwa likitumia kiwanda chake cha Utengenezaji wa Samani mbalimbali
kwa ajili ya matumizi ya Ofisi na hata nyumbani kilichopo katika Gereza la
Ukonga jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Kamishna
Msaidizi wa Jeshi la Magereza ambaye ndiye Mkuu wa Kiwanda cha Samani cha
Ukonga cha Jeshi la Magereza nchini kilichopo jijini Dar es Salaam John Itambu
anasema kwa sasa kiwanda hicho kinafanya
shughuli kubwa za aina mbili ikwemo
utengenezaji wa samani mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya ofisini na nyumbani
ikiwemo utengenezaji wa meza, viti, makabati,
vitanda, meza za chakula na za
ofisi, pamoja na meza za chumbani maarufu
kama ‘dressing table’.
Kamishna Msaidizi Itambu
anasema kiwanda hicho kinatengeneza samani hizo
kwa kutumia mbao za kawaida zile za asili zenye ubora wa kiwango cha juu
na zile za henzerani yaani miti ya minazi ambazo nazo pia zina mvuto wa hali ya
juu pia ikiwemo ubora pia.
Anasema pamoja na
utengenezaji wa samani kiwanda hicho pia kimekuwa kikijishughulisha na
utengenezaji wa kazi za mikono ikiwemo mazulia, vikapu, ‘table mates’ pamoja na
mazulia ya milangoni.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi
la Magereza Itambu ambaye ndiye msimamizi wa shughuli za Kiwanda hicho anasema
pamoja na kwamba Kiwanda cha Samani cha Magereza Ukonga kimekuwa kikitengeneza
samani zenye ubora wa hali ya juu lakini siku zilizopita kulikuwa na changamoto
ya ucheleweshaji wa ‘Oda’ ilikuwa mteja
akiagiza samani za aina fulani inachukua muda mrefu kukamilishiwa mahitaji yake
wakati mwingine na ubora unakuwa umepunguwa si kwa ubora aliokuwa ameuona
kwenye shughuli za Maonyesho ya Sabasaba.
Anasema kwa sasa Kiwanda
hicho kimeondoa changamoto hiyo ya ucheleweshwaji na sasa mteja anapoagiza mahitaji yake ya samani ziwe
kwa matumizi ya Ofisi au nyumbani mteja anapata mahitaji yake kwa wakati na kwa
ubora wa hali ya juu hakuna tofauti tena ya ubora anaotengenezewa na ule aliouona kwenye Maonyesho ya SabaSaba.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi
la Magereza John Itambu anasisitiza kuwa changamoto kubwa inayowakabili kwa
sasa ni ile ya bei za mbao kwa ajili ya kutengeneza samani zao kupatikana kwa
shida kwa kuwa mafundi wengi wa mitaani hununua mbao kwa kutumia fedha taslimu
na bila kupewa risiti za EFD sasa pale Jeshi la Magereza linapofuata taratibu
za kupewa risiti za EFD wauzaji wa mbao hutoa
kipaumbele kwa mafundi wale wa uraiani wenye fedha taslimu badala ya Magereza,
hivyo ni muhimu kwa Mamlaka husika kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na
wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kutumia mashine ama risiti za EFD.
‘‘Pamoja na kwamba mara
nyingi wateja wanaona bei za bidhaa za kiwanda chetu cha samani ziko juu lakini
wataalamu wetu wanachokiangalia ni kuzalisha bidhaa kwa kutumia mbao zenye
ubora wa hali ya juu miti hasa ile ya asili, na ndio maana samani zetu zinadumu
kwa muda mrefu huwezi kulinganisha ubora wake na bidhaa za mitaani’’
anasisitiza Mkuu wa Kiwanda hicho John Itambu.
Anasema kwa sasa kiwanda
kimeanzisha pia kitengo cha Masoko ndani ya Kiwanda chetu cha Samani ambacho
kinahusika zaidi na utafutaji wa masoko, pamoja na kusimamia oda zinazotolewa
na wateja wa kiwanda hicho ili ziweze kukamilishwa kwa wakati na ubora ule ule
waliouona wakati wa Maonyesho ya SabaSaba.
Hata hivyo Kamishna Msaidizi
John Itambu anatoa shukrani kubwa kwa Ofisi ya Rais Ikulu ambayo imekuwa ikiunga
mkono kiwanda hicho cha samani kwa kununua samani kwa matumizi ya ofisi hiyo, ikiwemo
pia ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Mali Asili
na Utalii.
‘‘Pamoja na Serikali kutoa
Maelekezo kwa Taasisi zote za Serikali kununua samani kwa ajili ya matumizi ya
ofisi kutoka kwenye Kiwanda cha Samani cha Gereza la Ukonga bado muitikio ni
mdogo bado hatujapata tenda kubwa kutoka kwenye ofisi za Serikali’’. Anaeleza
Mkuu wa Kiwanda hicho Kamishna Msadizi John Itambu.
Anasema mpaka sasa
wameshatengeneza samani za Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma, Mamlaka ya Chakula na
Dawa Tanzania (TFDA) pamoja na Ofisi za Bunge ambao waliotoa oda ya samani kwa ajili ya
ofisi za Wabunge kwenye Majimbo yao.
Pamoja utengenezaji wa
samani mbalimbali, Kiwanda chetu cha Samani Ukonga Magereza kina kitengo pia
kinachojishulisha na ushonaji wa nguo mbalimbali suti na mashati ya wanawake na
wanaume, ovaroli pamoja na sare mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya ofisi.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi
la Magereza John Itambu anasema kwa sasa Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha sare za
wafungwa 300 kwa siku, hivyo Kiwanda kina uwezo mkubwa wa kupokea tenda kubwa
kutoka kwa wateja mbalimbali hapa nchini.
Kamishna Msaidizi Itambu
anasema Kiwanda hiki cha Ukonga miaka mingi
iliyopita kilianza na shughuli za ushonaji wa nguo kwa kushona sare za majeshi
yaliyopo hapa nchini kwa kutumia wafungwa waliopo waliosimamiwa na Wataalamu
waliopo ndani ya Jeshi la Magereza na kwamba awali wazo kuu lilikuwa ni
kuwarekebisha wafungwa kwa njia ya kuwafundisha stadi za ushonaji baadae
kiliamua kuanzisha na shughuli za utengenezaji wa samani.
‘‘Awali tulikuwa tukishona
zaidi sare za Taasisi mbalimbali za Serikali kwa mfano sare za askari wa Jeshi
la Zimamoto na Uokoaji, askari wa Jeshi la Uhamiaji, kwa sasa Kitengo hiki kinachojishughulisha
na ushonaji wa nguo mbalimbali kimekuwa
kikipata tenda za kushona sare za madereva na makondakta wa daladala pamoja na
sare za askari wa Jiji la Dar es Salaam’’. Anasema Kamishna Msaidizi Itambu
ambaye ndiye Mkuu wa Kiwanda cha Samani cha Ukonga Magereza Jijini Dar es
Salaam.
Kwa upande wake Katibu Mkuu
wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Projest Rwegasira anasema
Kiwanda cha Samani cha Jeshi la Magereza kilichopo Ukonga jijini Dar es Salaam ni
moja kati ya viwanda vya hapa Tanzania vinavyotengeneza
samani zenye Ubora wa hali ya juu na ndio maana bidhaa zake zimekuwa zikidumu
kwa muda mrefu.
Meja Jenerali Rwegasira
anasema yeye binafsi ni miongoni mwa wateja wa Kiwanda hicho cha Ukonga na
amekuwa akinufaika na ubora wa samani zinazotengenezwa na Kiwanda hicho kwa
kuwa si kwamba zina ubora wa hali ya juu bali pia zinavutia kutokana na
wataalamu wake kuwa wabunifu na utaalamu wa kisasa katika utengenezaji wa
samani hizo.
Miongoni mwa wateja ambao
wamewahi kununua bidhaa hizo kwenye Kiwanda hicho cha Samani cha Ukonga,
Johnson Kapeu mkazi wa Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam anasema hivi ‘‘Kwa mara
ya kwanza nilihudhuria Maonyesho ya SabaSaba kati ya mwaka 2015 na
2016…nakumbuka nilihudhuria Maonyesho haya kama Mtanzania na Mtumishi wa Umma,
Rais Mstaafu Kikwete alipotembelea Banda la Magereza ndipo nami nikapata nafasi
ya kuona bidhaa za Magereza kweli nilivutiwa na baada ya hapo niliweka oda
yangu nikabahatika kupata samani nilizohitaji kwa wakati huo ilikuwa ni Kitanda,
Kabati la Nguo na Vyombo ambavyo hadi sasa ubora wake haujapungua hata kidogo.
’’ anasema Bw. Kapeu.
Kwa upande wake mmoja kati
ya wananchi ambao wamewahi kushiriki Maonyesho ya SabaSaba Edson Mandira mkazi
wa Ukonga jijini Dar es Salaam anasema “Ni kweli kabisa Jeshi la Magereza
linatengeneza bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na ikiwa wataalamu wake
watapata fursa za kutembelea Viwanda vya nje na ndani ya nchi wanaweza
kujifunza ujuzi mpya hivyo kuongeza ubunifu zaidi ambao utaendana na soko la
sasa ama ushindani wa soko la sasa kwa ujumla.
‘‘Mimi binafsi navutiwa sana
na ubora wa samani zinazotengenezwa na jeshi letu la Magereza ila wangeongeza
ubunifu kidogo tu… sasa ukichanganya na ubora wao wa hali ya juu wanaweza wakatuzidi
hata sisi mafundi wa Keko kwa kweli”. anasisitiza huku akicheka Bwana Gosbert Remanto ambaye ni fundi seremala Keko
DDC.
Kwa upande wake Ally
Abdulkarim mfanyabiashara wa samani eneo la Keko DDC anasema “Binafsi naona Samani
za kiwanda cha Magereza ni nzuri ila ndugu mwandishi wenzetu hawa wakiongeza
ubunifu kwenye “Finishing” na kuongeza ubunifu
wa kisasa … ndugu mwandishi wakifanikiwa hapo tu wenzetu hawa watafika mbali
sana na bidhaa zao zitatuacha tu … zitakimbiliwa hapa nchini kwa sababu ya
ubora wa hali ya juu, unajua hawa
wenzetu kwenye mbao sio wababaishaji kama sisi huku mtaani.
Naye Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini, Kamishna Jenerali Dk.
Juma Malewa anasema kuwa “Kutokana na Serikali kuhamishia Makao Makuu ya Nchi
yetu Mkoani Dodoma ni wazi kutakuwa na
uhitaji mkubwa wa samani kwa ajili ya matumizi ya ofisi na hata majumbani,
hivyo Jeshi la Magereza litajenga Kiwanda kipya kikubwa cha samani Dodoma ili kukidhi mahitaji halisi ya samani
hizo,’’ anasisitiza Dk. Malewa.
Dr. Malewa anasema ili kukidhi mahitaji halisi ya samani kwa ajili ya Makao Makuu ya
Nchi yetu jeshi lina mpango wa kununua vifaa hususani
mashine za kisasa zitakazoweza
kuzalisha samani kwa wingi zaidi na
hivyo kutosheleza mahitaji ya samani mjini Dodoma.
Hivi karibuni Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni, akikagua moja ya miradi ya Jeshi la Magereza
mkoani Dodoma alisema miradi mingi ambayo inaendeshwa na Jeshi la Magereza
nchini kikiwemo kiwanda cha samani cha Gereza
la Ukonga cha jijini Dar es Salaam, kama serikali itasaidia katika
kuiwezesha, italisadia taifa kupiga hatua na kuingia katika uchumi wa viwanda.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment