JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU
MAADHIMISHO YA SIKU YA FAMILIA DUNIANI MEI 15, 2018
Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani ambayo ufanyika
kila ifikapo tarehe 15 Mwezi Mei ya
kila mwaka, yataadhimishwa katika ngazi ya Mkoa hapa Nchini huku familia za
kitanzania bado zikikabiliwa na changamoto ya mila na desturi zenye madhara na
ukatili wa kijinsia na watoto ndani ya familia.
Taarifa ya vichocheo vya ukatili nchini ya mwaka 2015 inaonesha kwamba wanaotekeleza
vitendo vya ukatili ni watu wa karibu na familia au wanafamilia wenyewe. Aidha,
taarifa ya vitendo vya ukatili vilivyoripotiwa na Jeshi la polisi kwa mwaka
2017 vilikuwa 13,457.
Ili kukabiliana na madhara na changamoto zitokanazo na
vitendo hivi vya ukatili katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla Serikali
imeandaa kitini cha malezi kwa ajili ya
kutoa elimu malezi na hatimaye kupunguza matukio ya ukatili katika ngazi
ya familia.
Juhudi ya kutoa elimu ya malezi katika familia itasaidia
wazazi kuwa na mbinu za kuweka mazingira rafiki kwa watoto na ikiwa ni pamoja
na kutenga muda wa kutosha kukaa na kujadiliana masuala mbalimbali kwa lengo la
kujenga mahusiano yatakayowandaa kudumisha fikra za uzalendo, utu na maadili
mema katika kutumia familia zao na Taifa kwa ujumla.
Hadi sasa mafunzo hayo yametolewa kwa wazazi 3,600,
viongozi wa Serikali za vijiji 113, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa
Jamii Kutoka Halmashauri 76, wanafunzi 10,046, walimu 486, viongozi wa dini
110, wazee wa mila 90, ngariba 38 na
waendesha bodaboda 361.
Uelewa mdogo wa wanafamilia na jamii kuhusu malezi
yanayofaa kwa watoto na mbinu za kuimarisha mahusiano miongoni mwa wanafamilia huathiri
ukuaji wa watoto na kupelekea watoto kukosa mahitaji muhimu katika familia na
hatimaye kukimbia nyumbani. Kupitia kitini cha elimu ya malezi, familia
zitaweza kuboresha malezi na familia kuendelea kuwa mahali salama panapofaa
kuishi.
Kupitia Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi
ya Wanawake na Watoto 2017/18 – 2021/22, Wizara imeunda vikundi vya malezi na
kutoa elimu ya malezi katika familia 800 za mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya. Wizara
itaendelea kuhamasisha uundaji wa vikundi katika mikoa mingine ili kuimarisha
wajibu wa malezi katika familia.
Jamii imekuwa na mtazamo hasi kuhusu
malezi na hivyo kuongezeka kwa
mmomonyoko wa maadili kwa watoto na vijana. Utamaduni wa
familia tandaa kushirikiana katika malezi umekuwa ni changamoto kwa wakati huu
kutokana na kukosa mwitikio wa uwajibikaji katika malezi ya wanafamilia katika
jamii.
Matokeo
yake baadhi ya watoto wa mekuwa wanajilea wenyewe pale wanapofiwa na wazazi,
wazee nao wanakosa matunzo stahiki na wenye ulemavu wamekuwa wakitaarifiwa kufungiwa
ndani. Wakati tunaadhimisha Siku ya Familia Duniani kwa mwaka 2018, wazazi na
walezi wanatakiwa kuzingatia upendo na mahusiano mema ndani ya familia ili
kujenga familia na jamii iliyo bora na yenye maadili.
Siku
hii huadhimishwa na Nchi Wanachamawa Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa Tamko Namba
47/237 la Umoja wa Mataifa la tarehe 20 Septemba, 1993. Kwamatinki hiyo
madhumuni ya maadhimisho haya nikutambua umuhimu wa familia kama chanzo cha
jamii. Kaulimbiu ya
Maadhimisho ya mwaka huu ni “Malezi Jumuishi: Msingi wa
Uzalendo, Utu na Maadili ya Familia na Taifa”.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
(Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii)
13/05/2018
0 comments:
Post a Comment