Na: Hassan Hamad (OMKR) Hatimaye Chama Cha Wananchi CUF kimekamilisha mchakato wa kuchagua safu ya uongozi wa kitaifa kwa kuwachagua wajumbe 45 wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa, 20 kati yako wakitokea Zanzibar. Wajumbe hao ni miongoni mwa wajumbe 143 waliogombea Baraza Kuu la Uongozi (CUF) kupitia kanda saba za Tanzania Bara na mbili za Zanzibar ambazo ni Kanda ya Unguja na Kanda ya Pemba. Kuchaguliwa kwa wajumbe hao kumekamilisha safu ya uongozi wa kitaifa wa Chama hicho ambapo tarehe 25/06/2014 wajumbe wa mkutano mkuu wa CUF Taifa uliofanyika Ubungo Plaza Dar es Salaam, walimchagua tena Prof. Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho ambapo Maalim Seif Sharif Hamad alichaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho. Wajumbe hao pia walimchagua Mhe. Juma Duni Haji kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye amechukua nafasi ya Mzee Machano Khamis Ali ambaye hakuomba kugombea tena nafasi hiyo kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo ya kiafya. Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba, aliwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu kwa kuonesha nidhamu ya hali ya juu na kufanikisha uchaguzi huo kwa amani na usalama. Amesema hatua hiyo imedhihirisha ukomavu wa demorasia na uvumilivu ndani ya chama hicho, na kuwataka wajumbe waliochaguliwa kuendeleza kazi ya kukiimarisha na kukijenga chama hicho, ili kiweze kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wasiochaguliwa kwa upande wa Zanzibar, Mjumbe wa Mkutano huo Bi. Asha Ali Faki amesema wajumbe waliochaguliwa kuingia Baraza Kuu wana kazi kubwa ya kuwaunganisha wanachama, ili kuendeleza umoja na mshikamano uliopo ndani ya chama. Aidha amewanasihi wajumbe ambao kura zao hazikutosha kuingia katika Baraza hilo kutokata tama, na badala yake waunganishe nguvu zao kuweza kukabiliana na uchaguzi mkuu ujao. Akiwakilisha wajumbe waliochaguliwa kuingia katika Baraza Kuu la Uongozi CUF upande wa Zanzibar, Mjumbe wa Mkutano huo Bw. Salim Bimani amewashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kuwachagua, na kuahidi kushirikiana na wanachama pamoja na viongozi wa ngazi zote katika kukiendeleza chama hicho. Nae mjumbe wa mkutano huo akiwakilisha wasiochaguliwa kuingia Baraza Kuu kwa upande wa Bara Bw. Suleiman Bungala (Bwege), amesema wajumbe wa mkutano huo wamefanya maamuzi sahihi ya kuwachagua viongozi hao kulingana na maeneo wanayotoka. Amesema viongozi waliochaguliwa wameonesha umahiri mkubwa katika utendaji wao, na kwamba kazi kubwa inayowakabili hivi sasa ni kushirikiana na viongozi wengine pamoja na wanachama kuandaa timu ya ushindi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. “Viongozi tuliowachagua sasa tushirikiane kwa pamoja kuishinda CCM 2015”, alisema kwa madaha na majigambo. WALIOCHAGULIWA UNGUJA. Wajumbe kumi (10) waliochaguliwa kuwakilisha Baraza Kuu CUF kanda ya Unguja ni Salim Bimani, Nassor Ahmed Mazrui, Fatma Abdulhabib Ferej, Zahra Ali Hamad na Shaaban Iddi Ahmed. Wengine ni Pavu Juma Abdallah, Abdillahi Jihadi Hassan, Hassan Jani Massoud, Mohd Kombo Ali na Hemed Said Nassor. WALIOCHAGULIWA PEMBA. Kanda ya Pemba wajumbe 10 waliochaguliwa ni Hamad Massoud Hamad, Abubakar Khamis Bakar, Rukia Kassim, Said Ali Mbarouk na Khalifa Mohd Issa. Wengine ni Omar Ali Shehe, Riziki Omar Juma, Massoud Abdallah Salim, Hijja Hassan Hijja na Najma Khalfan Juma. WALIOCHAGULIWA BARA. Miongoni mwa wajumbe 25 waliochaguliwa kuingia Baraza Kuu la Uongozi (CUF) Taifa kwa upande wa Bara ni pamoja na Chifu Letalosa Yemba (aliyegombea Uenyekiti Taifa), Lobora Petro, Fatma Omar Kalembo, Magdalena Sakaya, Thomas Malima na Kapasha wa Kapasha. Wengine ni pamoja na Bonifasia Mapunda, Abdul Juma Kambaya, Ashura Mustapha, Karume Jeremia, Julius Nyanja Salim Sarwan na Katani Ahmed Katani. WALIOACHWA. Aidha wajumbe wa mkutano huo hawakuwapa ridhaa na kuwaacha baadhi ya wajumbe wa Baraza lililopita wakiwemo Khalifa Suleiman Khalifa, Mohd Habibu Mnyaa, Zakia Omar Juma, Joram Bashange na Khamis Hassan. Mapema akitoa maazimio ya mkutano huo, Mwenyekiti wa kamati ya maazimio Hassan Jani Massoud, alisema makubaliano ya marekebisho ya katiba yaliyofanywa kwenye mkutano huo yaingizwe kwenye katiba ya chama hicho ili yaweze kutumika kuanzia tarehe 22/08/2014. Kupitia maazimio hayo kamati hiyo pia imelitaka Baraza Kuu la Uongozi kusimamia haki ya watu wa kanda ya Kusini kuweza kufanya shughuli zao za kisiasa ikiwa ni pamoja na mikutano ya hadhara ambayo ilizuiwa na serikali. |
0 comments:
Post a Comment