Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akitembelea studio za (Azam TV) jijini Dar es
Salaam
Na: Hassan Hamad
(OMKR)
Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesifu mchango unaotolewa na
kampuni ya Azam, katika kukuza na kuendeleza sekta ya habari nchini.
Amesema kampuni hiyo
inayomilikiwa na mwekezaji mzalendo, imeonesha mafanikio makubwa tokea
ilipoanzisha kituo cha televisheni cha (Azam TV) takriban miaka miwili
iliyopita.
Maalim Seif ametoa
pongezi hizo wakati akitembelea studio za “Azam TV” jijini Dar es Salaam na
baadae kufanya mahojiano maalum na kituo hicho.
Amesema kituo hicho
kimeonesha ufanisi mkubwa wa kiutendaji na vitendea kazi, hasa ikizingatiwa
kuwa kimetoa kipaumbele kwa wafanyakazi wazalendo ambao wamepata fursa ya
kuendeleza taaluma na vipaji vyao.
Ametoa wito kwa
wawekezaji wazalendo kuiga mfano wa kampuni hiyo kwa kuwekeza miradi mikubwa
hapa nchini, ili iweze kuwasaidia vijana kuondokana na tatizo la ajira
linalowakabili.
Amesema hatua ya
wawekezaji wazalendo kuwekeza miradi mikubwa kama hiyo, pia inaijengea heshima
Tanzania katika jamii ya kimataifa na kuijengea mazingira mazuri ya ushindani
wa kibiashara katika soko la ajira.
Akizungumzia kuhusu
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais amesema imepata
mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kurejesha hali ya Amani, Utulivu na
mshikamano miongoni mwa wananchi.
Amesema amani iliyopo
ni hazina kubwa kwa Taifa, na kuwasisitiza wananchi kuienzi na kuilinda hazina hiyo ambayo
imelitengea sifa kubwa Taifa la Tanzania na wananchi kwa ujumla.
Amefahamisha kuwa
Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa itaendelea kuwepo hata baada ya uchaguzi mkuu
wa mwezi Oktobar mwaka huu, kwani imewekwa kikatiba na kwamba wananchi walio
wengi bado wana imani nayo kutokana na mafanikio yake.
Kuhusu utendaji wake
wa kisiasa, Maalim Seif ambaye tayari ametangazwa rasmi kuwa mgombea wa kiti
cha Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), amesema ameamua kuingia
tena kwenye kinyang’anyiro hicho akiamini kuwa bado anazo nguvu za kutosha,
uwezo na fikra mpya za kuwatumikia wananchi.
Kwa upande wake Naibu
Afisa Mtendaji Mkuu wa (Azam TV) Bw. Tido Muhando, amesema kampuni hiyo
imewekeza mitambo ya kisasa katika kituo hicho na kuwa na studio bora zaidi
katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema lengo la
kituo hicho ni kuwa na matangazo bora yatakayotolewa kwa lugha za Kiswahili na
Kiingereza kupitia (Azam TV 1 na 11) ambayo yatakidhi ushindani wa sekta ya
habari kitaifa na kimataifa.
Sambamba na hilo Bw.
Tido amesema kampuni hiyo pia inakusudia kuanzisha kituo cha Radio ndani ya
kipindi cha mwezi mmoja ujao, na kwamba masafa (frequency) ya radio hiyo tayari
yameshapatikana kwa upande wa Tanzania Bara
na Zanzibar.
Amesema
walishawishika kuanzisha vyombo vya habari kwenye kampuni hiyo baada ya
kuanzishwa timu ya soka ya Azam, na kuona haja kuitangaza kupitia televisheni.
Amefahamisha
kuwa kampuni hiyo inajipanga ili kuhakikisha kuwa inakidhi mahitaji ya wateja
wake katika ulimwengu wa soka kwa kuonesha mechi zote za kimataifa baada ya
kufanya mazungumzo na kampuni nyengine zinazoratibu matangazo ya aina hiyo. |
0 comments:
Post a Comment