SHULE YAWAZUIA ROBO TATU YA WANANFUNZI WAKE KUFANYA MITIHANI SHINYANGA, KISA MICHANGO!!
SHINYANGA, Tanzania
Katika
hali isiyokuwa ya kawaida robo tatu ya wanafunzi katika shule ya
sekondari Uhuru iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga wamezuiwa kufanya
mitihani ya muhula wa pili kwa madai ya wazazi wao kushindwa kulipia
michango mbalimbali.
Baadhi
ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo waliozungumza na waandishi wa
habari jana mjini hapa walisema pamoja na kuzuiwa kufanya mitihani hiyo
walimu wao waliwapa adhabu ya kukaa chini wakiwa juani na baadae
walipewa kazi ya kumwagilia bustani wakati wenzao wachache wakiendelea
na mitihani.
Mmoja
wa wanafunzi hao (jina tunalo) alisema walielezwa na walimu wao kwamba
ye yote ambaye hatokuwa amelipa ada na michango mbalimbali shuleni hapo
ikiwemo mchango wa mlinzi hatoruhusiwa kufanya mitihani hiyo mpaka pale
wazazi wao watakapokuwa wamelipa michango wanayodaiwa.
Mwanafunzi
huyo alifafanua kuwa hata pale walipojaribu kuwaomba walimu wawaruhusu
kufanya mitihani kwa vile suala la michango si jukumu lao bali la wazazi
waligoma huku wakibeza agizo la serikali lililotolewa hivi karibuni la
‘matokeo makubwa sasa’ (Big result now).
“Tuliwabembeleza
sana walimu waturuhusu kufanya mitihani hasa wale wa kidato cha nne na
cha pili kwamba matokeo ya mitihani hiyo kwa kawaida hujumuishwa na
matokeo ya mwisho ya kumaliza kidato cha nne na wale wa cha pili,
waligoma,”
“Binafsi
niliwaeleza kuwa hivi sasa serikali imetangaza mpango wa matokeo
makubwa sasa, lakini walimu hao walibeza na kueleza bila michango
kulipwa hakuna Big results now, tulishangaa, tukaambiwa wote ambao
hatujalipa michango na ada tukae chini uwanjani, hawakujali jua, kisha
tukapewa kazi ya kumwagilizia bustani,” alieleza mwanafunzi huyo.
Kwa
upande wake mkuu wa shule msaidizi Kasuka Masanja alikiri kuzuiwa kwa
watoto hao kufanya mitihani kutokana na wazazi wao kutokulipa michango
waliyotakiwa kulipa lakini hata hivyo alidai mitihani hiyo siyo halisi
bali ilikuwa ni majaribio ili kuwashinikiza wazazi kulipa ada na
michango wanayodaiwa.
Akizungumzia
hali hiyo ofisa elimu sekondari manispaa ya Shinyanga Victor Emmanuel
alishangazwa na taarifa za watoto hao kuzuiwa kufanya mitihani yao na
kwamba ni kinyume na maelekezo yaliyotolewa na serikali.
“Siamini
kama kweli wanafunzi hao wamezuiwa kufanya mitihani yao, si utaratibu,
suala la michango haliwahusu watoto, ni la wazazi na tuliishatoa
maelekezo ya jinsi ya kufuatilia michango hiyo kwa wazazi kwa utaratibu
wa kuwasiliana na viongozi wa serikali katika kata, hairuhusiwi kabisa
watoto kurudishwa nyumbani kwa kutolipa ada ama michango,” alieleza
Emmanuel.