THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
Kikwete: Kero hii imetosha, sasa ni kitabu kimoja mwanafunzi mmoja
·
Asema tunao
wanasiasa wa kutosha, sasa tunahitaji wanasayansi
·
Aaagiza
viongozi katika ngazi zote kutenga fedha za kuwajengea walimu nyumba katika
bajeti zao
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa
Serikali yake itakomesha kero ya wanafunzi na watoto wa shule nchini kuchangia
vitabu vya kiada katika masomo yao.
Aidha, Rais
Kikwete amesema kuwa wajibu wa kuhimiza ujenzi wa maabara za sayansi katika
shule nchini siyo tu matakwa ya Rais bali suala hili linatakiwa kuwa wajibu wa
kufa na kupona kwa kila kiongozi katika ngazi zote za uongozi kwa sababu nchi
haiwezi kuendelea bila wanasayansi.
Vile vile,
Rais Kikwete amewaagiza viongozi wote katika ngazi zote na hasa kwenye ngazi ya
wilaya na halmashauri kutenga katika bajeti zao fedha za kujenga nyumba za
walimu kwa nia ya kuboresha mazingira ya kazi ya walimu nchini.
Rais Kikwete
amesema na kutoa maagizo hayo jana, Jumatano, Oktoba 23, 2013, alipozungumza na
uongozi wa Mkoa wa Njombe wakati anakamilisha na kujumuisha ziara yake ya siku
saba katika Mkoa huo kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Rais ambaye
alizungumza masuala mengi kuhusiana na aliyoyaona wakati wa ziara hiyo
alijielekeza kwa muda mrefu katika masuala ya elimu na nafasi ya viongozi katika
kusuma mbele sekta ya elimu kama mkombozi mkuu wa Watanzania.
Kuhusu
kupatikana kwa vitabu vya kiada kwa watoto na wanafunzi nchini, Rais Kikwete
amewaambia viongozi hao wa Njombe:
“Nimeilekeza Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya ufundi kuwasilisha kwangu bajeti inayotakiwa kutuwezesha sisi, kama
Taifa, kuhakikisha kuwa kila mtoto wetu na mwanafunzi wa nchi yetu hii anakuwa
na kila kitabu cha kiada kwa kila somo.”
“Hili ni jambo
ambalo tumelizungumza kwa muda mrefu. Hakuwezi kamwe kuendelea kuahirisha majawabu
ya suala hili. Nataka kujua itatugharimu kiasi gani kwa kila mtoto na
mwanafunzi nchini kuwa na kitabu chake cha kiada kwa kila somo. Tumepata msaada
wa marafiki wetu. Tunawashukuru. Lakini sasa wakati umefika kwa sisi wenyewe
kuelekeza nguvu zetu zote kumaliza tatizo hilo,” amesema Rais
Kikwete na kusisitiza:
“Ilikuwa
wanafunzi 10 kwa kitabu kimoja, tumeshuka hadi wanafunzi watatu kwa kitabu
kimoja. Hili halitoshi na hali hii haikubaliwi ni lazima iwe ni mwanafunzi
mmoja na kitabu kimoja, kitabu chake.”
Kuhusu ujenzi
wa maabara ya sayansi katika kila sekondari nchini na umuhimu wa kufundisha
masomo ya sayansi nchini, Rais Kikwete amesema “ni lazima tujenge hizi maabara
haraka, ni lazima tuongeze kasi yetu ya kufundisha masomo ya sayansi na ni
lazima tukabiliane na uhaba wa walimu wa kufundisha sayansi nchini.”
“Maendeleo ya
nchi huletwa na wanasayansi. Na kama mfumo wa elimu wa nchi yoyote hautoi
nafasi ya kutosha kulea na kujenga wanasayansi basi nchi hiyo inapiga hatua ya
kurudi nyuma. Kwenye hili, tayari tumeachwa na treni na wala suala hili siyo
matakwa ya Rais bali ni suala la kufa na kupona kwa viongozi wote wa ngazi
zote,”
amesema Rais Kikwete.
Ameongeza: “Siyo
kila mtu katika nchi yetu atakuwa mwanasiasa. Hawa tayari tunao wa kutosha na
wengine kazi yao sasa ni kusababisha ghasia nchini. Tunahitaji wanasayansi
zaidi – tunahitaji madaktari, tunahitaji wahandisi. Ni lazima tuwekeze ipasavyo
katika eneo hili kwa sababu tukikosea sasa tutakuwa tumekosa hatua moja kubwa na
muhimu katika jitihada za kujiletea maendeleo.”
Amesema kuwa
anatambua matatizo yaliyoko katika ufundishaji wa masomo ya sayansi nchini na
kuwa kwa sababu hiyo ameitisha mkutano wa wadau wote wanaohusika na elimu na
eneo la sayansi nchini ambao utafanyika Novemba 3, mwaka huu, kwa nia ya
kutafuta majawabu ya matatizo hayo.
Tanzania
inahitaji walimu 44,007 wa sayansi katika shule zake za sekondari. Waliopo kwa
sasa ni walimu 17,059 na hivyo kuwepo na upungufu wa walimu 26,948 wakati vyuo
vyote nchini vina uwezo wa kuhitimisha walimu 2,100 kwa masomo ya sayansi kila
mwaka.
Kuhusu ujenzi
wa nyumba za walimu, Rais Kikwete amesema kuwa kila kiongozi popote alipo ni
lazima awe na mpango kabambe wa kuhimiza ujenzi wa nyumba za walimu na kuweka
katika bajeti yake ya kila mwaka fedha za ujenzi huo.
“Kwenye ngazi
ya taifa tumetoa Sh. Milioni 500 kwa kila Halmashauri nchini mwaka huu kama
namna ya kuanza kukabiliana na tatizo hilo. Mwaka huu wa fedha, tunaanza kwa
majaribio na Halmashauri 40 na ile ya Makete katika Mkoa huu wa Njombe ni mojawapo.
Tutaendelea kutoka fedha kila mwaka huu kwa nia ya kumaliza tatizo hili.”
Ameongeza: “Sasa
kwenye kila ngazi ya wilaya, kaeni chini mtafakari jinsi gani ya kuzitumia
fedha hizo vizuri ili ziweze kujenga nyumba nyingi. Natambua kuwa kwenye sehemu
nyingine shughuli hii itakuwa ngumu unapokuwa na madiwani ambao pia ni
wakandarasi. Lakini hii tutakabiliana nalo.”
Ameelekeza
kuwa mbali na kuzitumia fedha hizo vizuri, pia ametaka kila Halmashauri nchini
kutenga fedha katika bajeti zao za ujenzi wa nyumba za walimu.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.